Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA AFYA ATHIBITISHA KUPUNGUA KWA MAAMBUKI YA VVU, MKOA WA TANGA.Na Hamida Kamchalla, TANGA.


WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema maambukizi ya Virus Vya Ukimwi (VVU) yamepungua kwa Mkoa wa Tanga kutoka asilimia 4.4 ya Kitaifa na kufikia kiwango cha asilimia 2.9 hadi mwezi Disema 2023.

Waziri Mwalimu ameyasema hayo wakati akikabidhiwa vifaa vya kuboresha huduma za afya katika kupambana na magonjwa ya Vvu na kifua kikuu katika hospitali ya Rufani Bombo.


Vifaa hivyo ni pamoja na pikipiki 50, friji 72, centimetres 56, kompyuta 50, UPS 50 na printer 50 ambavyo vimegarimu kiasi cha sh. milioni 800, vimetolewa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa ufadhili wa serikali ya Marekani kupiyia kituo chake cha Kudhibiti na Kupambana na Magonjwa (CDC).


Kutokana na hali hiyo, amemtaka mganga mkuu wa hospitali hiyo Japhet Simeo kwa kushirikiana na watumishi wengine kuhakikisha wanaendelea kuhamasisha wananchi wa rika zote kupima VVU ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu.


"Habari nzuri ni kwamba maambukizi yamepungua katika Mkoa wetu, lakini hii isiwe sababu ya kujisahau, tunapaswa kila mmoja wetu kuchukua hatua na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya kuhusu namna bora ya kujikinga na maambukizi haya,


"Kila mwezi tuna wagonjwa wapya 300 kwa Mkoa huu wanaojiandikisha, kwahiyo Kitaifa siyo mbaya na ninaamini tunaweza kupunguza idadi ya watu wapya wenye maambukizi kwa kila mwezi" amesema.


Aidha Waziri ametoa maelekezo na kusema kuwa Wizara imejipanga kufikia asilimia 95 ya wagonjwa wanaojitambua hali zao kuwa na maambukizi Kitaifa ifikapo mwaka 2025 ambapo alibainisha kwamba mpaka sasa Mkoa wa Tanga umejitahidi katika makundi mawili kufikia malengo hayo.


"Mmefanya vizuri katika asilimia ya pili la vijana wenye umri wa miaka 19 hadi 24 ambayo mpo asilimia 97 na ya tatu la wanaume mpo asilimia 98, hongereni sana, sasa tuongeze nguvu kwenye kulifikia kundi la vijana kuanzia miaka 15 hadi 19,


"Lakini pia nataka nirudie tena kwa wanaume kupima VVU kuliko kusubiria majibu ya wake zao kwa kudhani ndiyo majibu yao, hapana, kila mmoja akapime na asubirie apate majibu yao" amesisitiza.


Kwa upande wa wakina mama wajawazito, Waziri alisema, "tunataka kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Kitaifa tupo asilimia 6.9 hivyo tunataka tufikie angalau chini ya asilimia 4 mwaka 2025".


Lakini pia ametaka kufikiwa kwa wanaotumia madaya ya kulevya na kujifunga sindano ili kuweza kupunguza maambukizi ikiwa ni pamoja na kuhimiza wananchi, "haya mambo yapo, tusione aibu kuyasemea kwakuwa tunataka kuwakomboa wananchi kuondokana nayo".


Waziri Mwalimu aliwaomba wafadhili wanaounga mkono juhudi za serikali kuwafikia wenye ugonjwa kifua kikuu kwa kushirikiana pamoja na jamii, viongozi wa dini na kimila lakini pia waganga wa jadi kutokana na utamaduni kwamba wananchi walio wengi hupenda kukimbilia huko.


"Ushirikishwaji wa viongozi hawa dhidi ya mapambano haya ni muhimu sana, muwakusanye , kila Wilaya na kuwapa elimu ya kutosha ili nao wakaeneze kwa watu walio karibu nao,


"Niendelee kuwashukuru sana wadau wetu hususani CDC katika kujitoa kwenu kuunga mkono juhudi za serikali katika magonjwa ya VVU, kifua kikuu na malaria, lakini pia mnatusaidia kutupitisha katika mifumo imara ya kuepuka magonjwa ya milipuko' amesema.

Post a Comment

0 Comments