Ticker

6/recent/ticker-posts

BRELA YAENDESHA MAFUNZO YA UELEWA DHANA YA WAMILIKI MANUFAA

Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau juu ya kuelewa dhana ya wamiliki manufaa 'Beneficial Owners' kwa lengo kuziwezesha kampuni kutuma taarifa sahihi.

Mafunzo hayo yamefanyika leo Machi 14,2024 katika ukumbi wa hoteli ya Seashells, jijini Dar es Salaam yakihusisha mawakili, wafanyakazi wa benki, wafanyabiashara na wadau wengine wa biashara.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu Robert Makaramba ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema kampuni nyingi si rahisi kumfahamu mmiliki wa kampuni au ubia, hivyo kupitia warsha hiyo wadau watapata uelewa juu ya kuwasilisha taarifa zinazotakiwa.

Jaji Mstaafu Makaramba amesema dhana ya wamiliki manufaa ni mpya na ilingia kwa kutumia sheria ya utakatishaji fedha, hatimaye imeingizwa kwenye sheria nyingine, ikiwemo sheria ya makampuni na uandikishaji majina ya biashara.

Amesema faida ya taarifa kuhusu wamiliki manufaa, inaimarisha biashara, kuvutia wawekezaji na kuondoa changamoto ya rushwa kwa sababu inahusu mmiliki halisi ambaye ni mtu.

"Nawapongeza BRELA kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuandaa warsha hii ambayo imekuja katika wakati muafaka, ni matumaini yangu washiriki wakitoka hapa watapata kile kitakachowaelewesha kuhusu wamiliki manufaa, amesema Jaji Mstaafu Makaramba.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara BRELA, Isdor Nkindi amesema kutokana na tathmini waliyofanya tangu kuanzishwa kwa sheria hiyo, bado kuna upungufu wa uelewa kwenye kuwasilisha taarifa ndiyo sababu wameamua kutoa elimu kwa wadau.

Ameeleza kuwa katika takwimu za sampo walizochukua 15,000 zilizowasilishwa, wamebaini upungufu wa uelewa wa dhana yenyewe na mipaka ya uwasilishaji ambapo zaidi ya asilimia 75 walikuwa wanafanya makosa katika ukokotoaji taarifa.

"Tunaendelea kuwajengea uwezo pale walipokwama na kuwaelekeza namna ya kuzirekebisha, tunatarajia kuanzia sasa na kwenda mbele, tunaamini taarifa zitakazofika kwa msajili zitakuwa zinasajiliwa moja kwa moja," amesema Nkindi.

Amefafanua kuwa dhana ya wamiliki manufaa ilikuja baada ya kuonekana kukuwa kwa kasi kwa makosa ya kifedha,iliyotokana na watu kujificha nyuma ya kampuni na makubalino, hivyo kushamiri makosa mbalimbali ikiwemo kupitisha fedha na bidhaa haramu.

Kwa upande wake mshiriki wa mafunzo hayo,Grad Mutani, amesema wamejifunza jinsi ya kutambua kuwa mmiliki wa manufaa lazima awe na hisa kuanzia asilimia tano na kuwataka mawakili kusaidia kuweka uwazi.

Post a Comment

0 Comments