Ticker

6/recent/ticker-posts

NAFASI YA KATIBU ITIKADI NA UENEZI RAIS SAMIA CHUKUA USHAURI WANGU

Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan

Na Said Mwishehe, 

NAFASI ya Katibu wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa iko wazi.

Sababu ya kuwa wazi ni baada ya Paul Makonda aliyekuwa katika nafasi hiyo kuondolewa na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa na Rais Dk Samia Samia Suluhu Hassan.

Iko hivi Rais Dk Samia amefanya mabadiliko katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ya kuwahamisha vituo vya kazi baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya.

Katika mabadiliko hayo ya baadhi ya wakuu wa mikoa ndipo Rais Samia akaamua kumteua Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha akichukua nafasi ya John Mongella ambaye taarifa ya Ikulu ilisema atapangiwa kazi nyingine. Hivyo kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa maana yake nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi iko wazi.

Kabla ya Makonda kuwa katika nafasi hiyo alikuwepo Sophia Mjema na kabla yake alikuwa Shaka Hamdu Shaka. Narudia tena nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi kwa CCM kwa sasa iko wazi .

Hata hivyo kipi kimesababisha Makonda kuondolewa katika nafasi hiyo kubwa ndani ya Chama hakuna anayejua zaidi ya Rais Samia mwenyewe. Tunaweza kutoa sababu nyingi na kueleza mengi lakini itakuwa ni mtazamo Wetu .Sasa kama aliyemuondoa hajasema, wewe uhalali wa kutoa sababu za kuondolewa kwa Makonda unatoa wapi.

Katika mitandao ya kijamii mengi yanazungumzwa kuhusu Makonda kuondolewa katika nafasi hiyo na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Wapo wanaodai kuwa huenda hotuba yake ya mwisho aliyoitoa wakati wa mapokezi ya ndege mpya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam itakuwa imesababisha . Binadamu tunajua kuunganisha mambo.Kha!!

Kwa kuwa nafasi hiyo iko wazi kwa vyovyote lazima ipate mtu ,lazima Mwenyekiti wake Taifa Dk Samia ateue mtu mwingine wa kuitumikia nafasi hiyo, nafasi ambayo ni muhimu katika Chama .Unapozungumzia Itikadi na Uenezi unazungumzia nafasi yenye maslahi mapana kwa Chama, ndio nafasi inayoweza kukisemea Chama, kukikana, kukipigania na kukitetea .

Nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama ndio sawa na mdomo wa Chama. Na hapo nimeeleza kwa juu juu tu. Ipo siku nitaizungumzia hatua kwa hatua lakini nilichofanya hapa ni kukupa picha tu ya unyeti wa nafasi hiyo.

Nikiri nafasi hiyo imetumikiwa na watu wengi na kwa nyakati tofauti lakini kwangu naweza kuizungumzia vizuri kuanzia Nape Nnauye ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Mtama na Waziri wa Habari.

Nape alikuwa katika nafasi hiyo enzi za Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Mwenyekiti wa Chama hicho Dk.Jakaya Kikwete. Wakati Nape akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Katibu Mkuu alikuwa Abdulurhaman Kinana.

Narudia tena kuanzia hapo ndipo naweza kuizungumzia nafasi hiyo, nafasi ambayo inahitaji mtu mwenye uwezo mkubwa na maarifa kichwani.Ndio,kukisemea Chama kama CCM sio jambo dogo. Inahitaji mtu machachari lakini anayejua nini anatakiawa kufanya kwa maslahi ya Chama na Watanzania kwa ujumla .

Kwa Nape aliifanya kazi yake vizuri,Sitaki kuwapanga kwa ubora lakini Narudia tena Nape aliiweza nafasi hiyo.Najua baada ya Nape aliyekuwa Humphrey Polepole kushika nafasi hiyo katika Serikali ya Awamu ya Tano .Naye alifanya kazi yake na baadae akaja Shaka Hamdu Shaka.

Hakika Shaka hakuwa na shaka katika nafasi hiyo,alitimiza majukumu yake na baadae akawekwa kando na nafasi hiyo akapewa Sophia Mjema. Dada Sophia naye aliitumikia nafasi hiyo kwa kadri alivyoweza na baada ya kuondolewa ndipo akaja Makonda.

Kijana anayejua siasa za mtandaoni,siasa za majukwaani ,siasa za kishua,siasa za kibabe.Kuteuliwa kwa Makonda kukawa na maneno mengiiii, wapo waliosema Chama kimepata mtu .

Na Makonda kama unavyomjua alipo lazima watu wake, mapokezi yake katika ofisi za Lumumba yalikuwa ya aina yake.Msela aliingia na bodaboda hadi Lumumba.Jamaa anajua kutengeneza matukio yanayofanya lazima azungumziwe

Hajakaa sawa akatangaza kuanza ziara mikoa 10,ziara ambayo aliifanya,katika ziara yake aliamua kuchukua waandishi kutoka vyombo mbalimbali na kwa kuwa siasa za mtandaoni anazijua akaamua kuchukua waandishi wa habari za mtandaoni,wanaitwa.Blogger na social media.

Watanzania wakaanza kushuhudia ya Makonda ziarani,akatatua shida za watu,akatoa maelekezo kwa Mawaziri wa Serikali,wakuu wa mikoa na Wilaya,wabunge na watendaji wengine wakuu wa taasisi.Utaratibu wake ulilalamikiwa na baadhi ya wanasiasa ambao wanaamini katika kutekeleza majukumu kwa kuheshimu Katiba ya Chama,kanuni na taratibu.

Hata hivyo lengo langu si kuzungumzia yaliyofanywa na Makonda,ila naandika tu kuweka angalizo kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk Samia Suluhu Hassan wakati anafikiria nani awe Katibu wa Itikadi na Uenezi ni vema akafikiria na nani anaweza kufiti katika nafasi hiyo kwa sifa na vigezo.

Najua RAIS anautashi wake katika nafasi hiyo lakini niombe na nimkumbushe asilimia kubwa ya Watanzania kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi nchi yetu inavijana wengi kuliko wazee.Huo ndio ukweli,rejea ripoti ya sensa iliyotolewa na Serikali yetu.

Hivyo pamoja na sifa zote ukweli anahitajika Katibu wa Itikadi na Uenezi ambaye atakuwa anajua kuishi na vijana ambao ndio wengi.Anahitajika Katibu wa Itikadi na Uenezi ambaye anajua kuzungumza lugha za vijana, Katibu wa Itikadi na Uenezi anayejua apite wapi atokee wapi kwa vijana.

Akipatikana Katibu wa Itikadi na Uenezi kijana naamini CCM itakuwa imejenga daraja kati yake na vijana wa nchi hii ambao wenyewe wanaamini ndio Taifa la leo na sio Taifa la kesho.Kikubwa ni kuwa na kijana mwenye sifa, maarifa,uelewa lakini kubwa zaidi kuwa na kijana mwenye hekima na busara.

Ujue kwenye nafasi kama Katibu na Uenezi mbali ya kuwa namsha aamsha lazima hekima na busara itawale .Ukiwa na kijana halafu Hana hekima ,hana busara Chama kitajiweka katika wakati ngumu.Ndio mbona mifano ipo.Unataka nikutajie wakati Mwenyewe unaijua.

Nimeona yameanza kutajwa majina mengi ya warithi wa Makonda katika nafasi hiyo,Sina shaka na uwezo wao,wengi nafahamu uwezo wao, uzalendo wao kwa Chama na Serikali,wanaiweza nafasi hiyo lakini kwa umri wao nadhani sio wakati sahihi kwao,sio kwamba hawawezi lahasha,wanaweza lakini watakosa lugha za kuwasiliana na kizazi cha sasa.

Ndio maana ushauri wangu kwa Rais Samia ni vema akafanya utafiti wake,akachunguza pande zote za Chama na kisha akaja na kijana,ila asiwe kijana oyaa oyaa bali awe kijana aliyetimia.

Kijana ambaye anaweza asiwe kijana atakayeingia na tingatinga uwanjani lakini kijana anayejua wajibu wake,anayejua Chama kinataka nini na wakati gani.Kijana anayejua aseme nini ? Kwanani na wakati gani.Sio kuwa na kijana ambaye yuko mkutanoni anatatua shida za watu lakini akili inawaza Beach Kidimbwi.

Nakuamini Rais Samia utateua mtu sahihi kwa ajili ya nafasi hiyo,mtu ambaye atatimiza majukumu ya Chama hasa katika mwaka huu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwakani Uchaguzi Mkuu.

Sina shaka na Rais Samia, Rais anayefanya mambo yake kwa utulivu.Kwa lugha rahisi ni vema Rais Samia ukatuteulia Katibu wa Itikadi na Uenezi kijana lakini anaaweza kuzitafsiri vizuri zile R nne zako .

Naomba nihitimishe hivi, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Dk.Samia Watanzania wanaimani kubwa na wewe, Watanzania wanakupenda,wanakuthamini na katika mioyo yao wamekuweka wewe .

Wako pamoja nawe na wako pamoja nawe zaidi katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025, wanataka kukuona unashinda kwa kishindo.Sio wao tu hata Mimi niko na wewe tu.Tuletee Mwenyezi mzuri tuampa ushirikiano.

Halafu Rais wangu naomba hili nichomekee kwako,wananchi wako wa Majohe Kwangosoma,Majohe Halisi hadi kwa Mpemba changamoto yetu kubwa ni barabara,tunaomba barabara ya lami,tumeahidiwa kwa muda mrefu.

Nikuombe Rais wetu tusaidie barabara hiyo inayoanzia eneo la Pugu sekondari Nikushukuru kwa mita 400 ambazo tumewekewa lami na taa za juu lakini tutashukuru zaidi ukitukamilisha.

Na Mwenezi utakayemteua tunaomba ziara yake ya kwanza iwe Majohe kwasonga.Atafikaje? Jibu ni kwamba Mbunge wa Jimbo la Ukonga na Waziri wa Aridhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jery Silaa anapajua vizuri,atamleta.


Kasimu kangu
0713833822

Post a Comment

0 Comments