Ticker

6/recent/ticker-posts

WANA CCM TUSIBWETE, UCHAGUZI UTAKUWA NA USHINDANI-KINANA

Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Rorya

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana ameshauri wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kutobweteka katika mwaka huu wa Uchaguzi wa serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu mwakani kwani uchaguzi utakuwa na ushindani mkubwa.

Akizungumza na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Rorya mkoani Mara Kinana amewakumbusha wanachama wa Chama hicho kujipanga kikamilifu ili kuibuka na ushindi katika chaguzi hizo.

Amesema kuna kanuni za uchaguzi za vyombo vya dola, hivyo wanatakiwa kufuata maadili ya uchaguzi na wafanye kila linalowezekana kwani amepata ahadi nyingi kuwa watashinda katika uchaguzi unaokuja wa Serikali za mitaa mwaka huu.

“Niwaambie uchaguzi utakuwa na ushindani kwasababu zile sheria za uchaguzi zilizotungwa bungeni zinatoa nafasi ya ushindani.Kwahiyo tusibwete, badala yake tujipange vizuri.

“Tunatakiwa tujipange wanachama ili tupate ushindi wa kishindo mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2025,” amesema na kusisitiza kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa ni vema wana CCM wakashikamana.

“Kama kuna mtu mchana yuko upande wa CCM na usiku upinzani anapaswa kuwekwa kando haraka.Hatuwezi kukubali watu wavae nguo za kijani mchana halafu baadaye unabadilika, hatuwezi kukubali,” amesema.

Makamu Mwenyekiti Kinana ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Mara ametumia nafasi hiyo kueleza ni muhimu kuendeleza umoja na mshikamano na kama kuna changamoto wanapaswa kuzizungumza ili kupata ufumbuzi.

Akizungumzia viongozi waliochaguliwa na wananchi na sasa wako madarakani wakiwemo madiwani na wabunge amesema waachwe wafanye kazi na wala hakuna sababu ya kuwavuruga.

“Kuna watu wanaitwa madalali wa vyeo, kazi yao ni kuuza vyeo anakuja kwako anakwambia mwaka ujao unatakiwa tukuchague wewe, ukisikia hivyo ujue anatafuta riziki na akimaliza kuzungumza anaomba nauli, ujue huyo ni dalali.

“Wakati mwingine anakupigia simu anakwambia hebu nirushie bando kuna habari nataka nikupe. Hao ni madali, ukija kuanguka anasema mimi nilikusaidia ila wajumbe wamekuangusha.” alieleza.

Ameongeza kwa kipindi cha uchaguzi bado hakijafika kuna watu wanatamaa ya kuwa madiwani, ingawa tamaa sio dhambi maana ndio hulka ya binadamu lakini ni muhimu utaratibu wa Chama na kanuni mbalimbali ziheshimiwe na walioko katika uongozi waachwe wafanye kazi.

Post a Comment

0 Comments