Na Hamida Kamchalla, TANGA.
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya nchini imejikita kuanzisha huduma za utengamao kwa watu wenye mahitaji maalumu hususani walemavu wa viungo katika hospitali zote za rufani za Mikoa na Wilaya ili watoto wote wenye ulemavu waweze kupata huduma hizo.
Mpango huo utaanza kutekelezwa mara baada ya kukamilika kwa programu ya mafunzo ya shahada ya kwanza ya huduma kazi katika chuo cha Muhimbili ambayo inaanzishwa chini ya serikali ya awamu ya sita.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Godfrey Mnzava katika kituo cha watoto wenye ulemavu cha YDCP jijini Tanga wakati mwenge huo ulipotembelea mradi wa kazi za mikono za utengenezaji wa urembo na mapambo mbalimbali wa watoto wenye ulemavu wa viungo kituoni hapo.
Waziri Mwalimu amesema kituo hicho kwa kushirikiana na wadau wa Afya pamoja na halmashauri ya jiji la Tanga kinatekeleza huduma hiyo, lakini hazipatikani katika Wilaya zote za Mkoa huo.
'Kwa sababu ya mapenzi makubwa na utu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunakwenda kuanzisha huduma hizi katika hospitali zote za rufani za Mikoa na Wilaya nchi nzima ili kuhakikisha watoto wote wenye ulemavu wanafikiwa na huduma hii",
"Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu tumeanzisha Shahada ya huduma kazi, lakini pia tumeanzisha mafunzo ya Stashahada ya lugha ya mawasiliano kwa vitendo, kwahiyo baada ya miaka mitatu tutakuwa na wataalamu hawa nchi nzima na tutawasambaza katika maeneo yote" amesema.
Kuusu dawa za kulevya, Waziri Mwalimu amesema kupitia serikali, jiji la Tanga limewawezesha vifaa mbalimbali vya kufanyia kazi viajana ambao wanatumia dawa za methadone na kuachana na uraibu wa dawa hizo ili waweze kujitafutia kipato chao na kuachana na makundi mabaya ya ushawishi.
"Mimi kama mbunge kupitia serikali tumewapa masine za kuosha magari, mashine za kufyatulia matofali na cifaa mbalimbali, kwa sababu wajibu wetu kama jamii ni kutowaadhibu watu wanaotumia dawa za kulevya kwasababu wao ni wahanga" amebainisha.
Naye Ofisa Ustawi wa jiji la Tanga Hossein Mshana amebainisha kwamba kituo cha YDCP kwa sehemu kubwa kinaendeshwa na michango ya jamii, wafadhili pamoja na serikali ya Mkoa.
"Lengo la kituo hiki ni kutoa huduma za msingi za utengamavu, lishe, kuzuia na kupinga ukatili wa kijinsia, ujumuishi na ushirikishwaji wa vijana na watoto wenye ulemavu katika jiji latu la Tanga" amesema.
Mnzava amebainisa kwamba kituo kimefanikiwa kuwafikia watoto 2,368 ambapo wakike ni 1,236 na wakiume ni 1,132 wenye ulemavu na huduma za utengemavu ikiwa ni pamoja na mazoezi tiba na vifaa visaidizi.
Amesema yapo makundi mawili ya wazazi wenye watoto wanaoishi na ulemavu wameweza kusaidiwa kiasi cha sh milioni 18 kutoka katika mapato ya ndani ya halmashauri, ikiwa ni pamoja na vijana 6 wenye ulemavu wamewezeshwa na mkopo wenye thamani ya sh milioni 6.5 na tayari wameshaanza kurejesha kwa asilimia 77.
"Lakini pia kituo kimesaidiwa na halmashauri kwa kupatiwa wataalamu wanne ambapo watatu ni kwa ajili ya viungo bandia na mmoja ni wa tiba kazi, na mpaka sasa kituo kimeweza kuboresha miundombinu rafiki kwa watoto katika shule mbili za msingi za Magaoni na Kisosora" amesema.
Kwa upande wake mkimbiza mwenge wa uhuru Kitaifa Godfrey Mnzava ameupongeza uongozi wa kituo hicho kwa hatua nzuri ya utoaji wa huduma za utengamao kwa watoto hao, lakini pia mradi ulioanzishwa kwani unawawezesha kujituma na kupata ujuzi utakaowasaidia kuingiza kipato chao.
Mnzava amezungumzia suala la dawa za kulevya katika Mkoa wa Tanga huku akiitaka jamii kuungana kwa pamoja na kuhakikisha wanapambana na kudhibiti matumizi ya dawa hizo kwa vijana.
'Matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa tatizo kubwa kwa jamii, jambo ambalo jamii isipoungana kwa pamoja na kupiga vita litasababisha madhara makubwa kwa vijana ambao ndiyo nguzo ya Taifa letu" amesema.
0 Comments