Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT .BURIANI ATAKA WAHAMIAJI HARAMU WADHIBITIWE MPAKA WA HOROHORO.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani akiongea na viongozi wa kituo cha Forodha cha mpaka wa Horohoro.
Dkt Buriani akipokea taarifa ya kituo cha Horohoro kutoka kwa Ofisa Mfawidhi wa kituo hicho  Shadrack Mbonea.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani akiongea na viongozi wa kituo cha Forodha cha mpaka wa Horohoro.

*********************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka viongozi wa kituo cha mpaka wa Horohoro kuweka ulinzi madhubuti mpakani humo kuhakikisha wanazuia upitishwaji wa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.

Dk. Buriani ameyasema hayo alipotembelea kituo hicho katika ziara yake ambapo alibainisha kuwa kumekuwa na tabia ya wahamiaji kuingia nchini kwa njia za panya hivyo ni wajibu wa viongizi kuwa hao kuwa makini.

"Nitoe wito kwenu viongozi, mnatakiwa kuwa makini sana katika mpaka huu kuhakikisha isiwe njia ya kupitishia wahamiaji haramu kuingia mkoani kwetu,

"Lakini pia fanyeni ukaguzi kuhakiki vizuri magari yanayovuka hapa, siku hizi hadi makontena ya kubebea mafuta yanatengenezewa viti ndani kwa ajili ya kuwavusha wahamiaji haramu" amesema.

Awali akisoma taarifa ya kituo hicho Ofisa Mfawidhi wa kituo hicho Shadrack Mbonea amesema kituo hicho kinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa baadhi ya vifaa kama Scanner ya Mizigo mikubwa, pamoja makazi ya watumishi.

"Pamoja na matatizo yanayotukabili lakini tumeweza kufanikiwa kuvuka lengo katika ukusanyaji wa mapato ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024 kituo kimekusanya sh bilioni 68.5, sawa na asilimia 117.18 ya lengo" amesema.

Katika ziara hiyo, Dkt. Buriani pia ametembelea bandari ya Tanga ambapo ameupongeza uongozi kwa mwanzo mzuri kiutendaji baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali katika bandari hiyo.

Amebainisha kwamba serikali ya Mkoa huo ina nia na lengo thabiti kuleta maendeleo yenye tija kupitia bandari hiyo hasa kupitia Wizara ya kilimo katika mazao ya kimkakati.

"Mmeanza vizuri sana, tunampongeza Rais wetu kwa uwekezaji huu mkubwa alioufanya, Wizara ya Kilimo itatumia sana bandari hii kwa kusafirishia mazao yetu ya kimkakati ikiwemo katani na chai,

"Tutaendelea kushirikiana kuutangaza Mkoa wetu kupitia bandari hii, sisi kama Mkoa tutakuwa na banda letu kuonesha vitu vilivyopo, ikiwa ni pamoja na bandari hii" amefafanua.

Naye Kaimu Meneja wa Bandari Tanga Peter Milanzi alieleza kuwa uboreshwaji wa bandati hiyo umefungua milango ya biashara katika Mkoa wa Tanga na kwa sasa ina uwezi wa kuhudumia meli 3 kwa wakati mmoja.

Milanzi amesema ndani ya kipindi cha miaka minne idadi ya meli zilizohudumiwa bandarini hapo imeongezeka kutoka kwa asilimia 16.2 ambapo mwaka 2018/ 19 kabla ya uboreshwaji zilihudumiwa meli 125 na mwaka 2022/ 23, zilihudumiwa meli 195 baada ya uboreshwaji.

Amebainisha kwamba ongezeko la abiria wanaotumia bandari hiyo ilipungua katika kipindi cha mwaka 2021/ 22 idadi ilipungua baada ya meli ya kampuni ya Azam iliyokuwa ikifanya safari zake kuharibika.

"Kwa kuona tatizo hilo la kupoteza wateja, kiasi cha shilingi bilioni 429.1 ziliwekezwa na serikali katika miradi miwili ya kuboresha bandari yetu,

"Mradi wa kwanza ulihusisha kuongeza kina na kupanua mlango wa kuingia na kutoka kwa meli ambao ulitumia kiasi cha sh bilioni 172.3, na sh bilioni 256.8 zilitumia kwa mradi wa uchimbajibwa kina kwenye mlango wa bandari na sehemu ya kugeuzia meli" amefafanua.

Post a Comment

0 Comments