Ticker

6/recent/ticker-posts

FANYENI KAZI KWA MALENGO BILA KUVUNJA SHERIA.

Waendesha pikipiki maarufu bodaboda wa kijiwe cha Mtakuja kilichopo njia panda ya Iyula Kitongoji cha Luwemba Kata ya Ruanda wametakiwa kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi bali watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili ziweze kushugulikiwa.

Rai hiyo imetolewa Mei 13, 2024 na Polisi Kata ya Ruanda Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Happy Lumbe alipowatembelea bodaboda hao kijiweni hapo na kuwapa elimu ya madhara ya kujichukulia sheria mkononi.

“Acheni kujichukulia sheria mkononi pindi mnapopata changamoto kwenye kazi zenu za kila siku endapo utafanyiwa kitendo cha ukatili au uhalifu unatakiwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, msimpige mhalifu mpaka ukamuua hilo ni kosa la jinai acheni sheria ichukue nafasi yake na ahukumiwe kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine” alisema Mkaguzi Lumbe.

Sambamba na hilo mkaguzi Lumbe amewasisitiza bodaboda hao kuzingatia sheria zote za usalama barabarani pale wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto kwani kufanya hivyo kutawaepusha na ajali zinazoweza kuepukika na kuendelea kuwa salama katika majukumu yao ya kila siku.

Aidha amewaasa kujiunga katika vikundi vya Ulinzi Shirikishi ili kuimarisha ulinzi katika maeneo yao na kudhibiti vitendo vya kihalifu katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments