Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI IMEJIPANGA KUBORESHA ELIMU, AJIRA ZA KUJUANA ZIFE.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

SERIKALI imesema ina kazi kubwa ya kuendelea kutenga bajeti kila mwaka kuhakikisha wanaboresha walimu wote nchini ikiwa ni kuwapa fursa ya kujiendeleza pamoja na kuwajengea uwezo zaidi kielimu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akifungua mkutano wa Uwasilishaji wa Taarifa ya Tathmini ya Ujifunzaji na Ufaulu wa Wanafunzi Mkoa wa Tanga.

Prof. Mkenda amefafanua kwamba wakati serikali inaendelea na kufanya maboresho hayo Kwa walimu waliopo, walimu ambao watakuja kuajiriwa inawapasa kuingia kwanza darasani na yule ambaye atafanya vizuri zaidi ndiye atakayepatiwa ajira.

"Ajira hii tusiangalie kama ni fursa ya kwamba mwanangu ameajiriwa badala yake tuangalie kama mwanangu amepata mwalimu bora, kama tukiiangalia kuwa fursa ya kuajiriwa tunagombana bure, hizi nafasi ni chache" amesema Prof. Mkenda.

"Na sisi tunazalisha walimu wengi na fursa za ajira huwa ni chache mno kuliko wanaotaka kuajiriwa, kwahiyo tunatumia kigezo ambacho kitatuvusha na kuvusha Taifa letu" amebainisha.

Aidha amesema serikali itahakikisha inaajiri walimu ambao wanafanya kazi hasa kwa kuondoka shinikizo la watu kupeana kazi mazoea ya kujuana na kusaidiana kwenye taaluma ambazo zinahitaji kusomea na kufaulu kikamilifu.

"Haiwezekani mtu aje tu akwambie samahani nina mtoto wangu amesomea ualimu lakini hajafaulu anahitaji kazi, na akipata tuna uhakika gani kama kweli aliyepata ataweza kuwa bora kuliko yule aliyeachwa,

"Tathmini hii na kama kweli tunataka elimu yetu iendelea lazima twende kwa ujasiri, tunapotaka kuajiri mwalimu wetu ni lazima kwanza tujiulize, tunapigania ndugu na watoto wetu wapate ajira au ndugu na watoto wetu wapate elimu bora" amesema.

Hata hivyo Prof. Mkenda amebainisha kwamba ipo haja kufanya utafiti katika shule zilizopo maeneo ya vijijini ambazo miaka yote zimekuwa hazina matokeo ya kuridhisha.

"Kuna haja ya kufanya tafiti Ili kujua kama tatizo ni umbali wa shule au walimu wake siyo wazuri, Maofisa Elimu wa Mikoa, najua mna kazi kubwa sana mnayoifanya kwenye maeneo yenu,

"Niwaombe huko katika Mikoa yenu muendelee kusaidia serikali Kwa ajili ya kuongeza ubora wa mitaala lakini pia kuongeza uboreshaji katika ufundishaji" amesisitiza.

Naye Katibu wa Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dkt. Said Mohamed akiwasilisha Tathmini ya Ujifunzaji na Ufaulu wa wanafunzi Kitaifa amesema takwimu zinaonesha usjali umeongezeka.

Dkt. Mohamed amesema mwaka Jana somo la hisabati ndiyo liliongoza pekee kwa asilimia 25 ingawa bado iko chini na kwamba ni asilimia 5 pekee ndiyo imeongezeka kutoka asilimia 20 mwaka jana.

"Kwa kipindi Cha miaka kumi mfululizo, kuanzia mwaka 2015 hadi 2023 tuko kwenye rangi nyekundu kwamba tuko chini ya wastani wa Kitaifa, na hakuna Mkoa uliofaulisha zaidi ya asilimia 30" amesema.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani amesema yapo baadhi ya masomo ya sayansi hayaridhishi katika Mkoa huo, na kwamba kukutana kwa wadau hao inaleta imani kwamba wataboresha pale penye shida.

Post a Comment

0 Comments