Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZALISHAJI WA VYAKULA VYA MIFUGO WAPEWA ONYO, SHERIA KUWAKABILI

Serikali imewataka wazalishaji na wasambazaji wote wa rasilimali na vyakula vya wanyama kuhakikisha vyakula na viwanda vyao vimekaguliwa na kufikia na ubora na usalama unaohitajika.

Hayo yamesemwa leo (31/05/2024) jijini Arusha wakati wa kuhitimishwa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ya wakaguzi wa vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), baada ya kufanya ukaguzi katika baadhi ya viwanda, wauzaji wa vyakula vya mifugo na kuwatembelea baadhi ya wafugaji wanaotumia vyakula hivyo.

Akiongoza timu ya ukaguzi, Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka TVLA Dkt. Zacharia Makondo amesema ni muhimu kwa vyakula vya mifugo kufika sokoni kama vilivyowekwa viwandani na wale ambao wanapuuza suala la kupima na kuhuisha usajili wa viwanda vyao watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama.

Dkt. Makondo ameongeza katika utekelezaji wa zoezi hilo, wale wote ambao hawajasajiliwa watawafungia na hawataruhusiwa kufanya shughuli hiyo, huku akibainisha kuwa maabara za kanda zitawezeshwa kuwa na vifaa vya kufanya ukaguzi katika maeneo ambayo yanauhitaji mkubwa wa kufanywa kwa ukaguzi wa rasilimali za vyakula na vyakula vya mifugo ili kuhakikisha vinakuwa salama.

Aidha, amesema baada ya kufanya zoezi hilo kwa ufanisi katika Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kaskazini, zoezi hilo litafanywa kwenye kanda zingine kwa ajili ya kuendelea kukagua pamoja na kufanya uchambuzi wa vyakula na rasilimali za vyakula vya mifugo.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Mifugo, Idara ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Theodata Sallema, amesema wizara inawakumbusha wakaguzi kufanya ukaguzi katika maeneo yao na kuhakikisha wadau wanafuata sheria.

Bi. Sallema amebainisha kuwa wale ambao wanafunga vyakula vya mifugo au madini katika vifungashio vidogo wahakikishe vinakuwa na lebo na maelezo ambayo yanaendana na mfuko wa awali ambao wameufungua kwani kwa kutofanya hivyo ni kinyume cha sheria na kuashiria udanganyifu.

Pia, amesema wizara inaendelea kuwashukuru wadau kwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria zilizowekwa na kwamba changamoto zilizobainishwa zitawasilishwa kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Naye Meneja wa TVLA Kanda ya Kaskazini – Kituo cha Arusha, Dkt. Rowenya Mushi amesema kanda hiyo ambayo inahudumia mikoa mitatu ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro imepata chachu ya kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa wazalishaji na wasambazaji wa vyakula vya mifugo juu ya kupima vyakula vyao kuwa na ubora na kuleta matunda kwa wafugaji.

“Chakula bora huwa kinaleta mazao bora kwa wafugaji na hilo ndio lengo kuu la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na serikali kwa ujumla, kuhakikisha mfugaji anafuga kisasa na kupata chakula bora kwa ajili ya mifugo yao hatimaye kupata mazao bora na kupata kipato kizuri zaidi na kukuza uchumi.” Alisema Dkt. Mushi

Sambamba na hilo amewasihi wazalishaji wa vyakula vya mifugo kufikisha sampuli ya vyakula vyao katika maabara ya TVLA katika kila toleo kuhakikiwa ubora na kupatiwa elimu na ushauri juu ya vyakula hivyo ili kuleta tija kwa wafugaji wanaotegemea vyakula hivyo.

Baadhi ya wadau wa kuzalisha na kusambaza vyakula vya mifugo pamoja na wafugaji wanaotumia vyakula hivyo, wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa kufanya ukaguzi na kuwafafanulia mambo kadhaa yanayohusu vyakula hivyo ili kuimarisha ubora pamoja na kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.

Wameiomba serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutenga muda zaidi wa kufanya ukaguzi zaidi ili kuviondoa sokoni baadhi ya viwanda ambavyo vinazalisha vyakula hivyo katika ubora wa chini na kuwauzia kwa bei ndogo wafugaji wakidhani wamepata unafuu wa bei na kuwasababishia wafugaji kutopata matokeo mazuri ya mazao ya mifugo hiyo.

TVLA inatarajia kuendelea kutoka elimu na kufanya ukaguzi wa rasilimali na vyakula vya mifugo katika kanda mbalimbali za wakala hiyo pamoja na kusimamia sheria ili wafugaji ili waweze kufuga kwa tija na kupata matokeo bora kupitia ufugaji.
Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo (wa pili kushoto) akitoa elimu ya umuhimu wa upimaji wa virutubisho vinavyoongezwa kwenye vyakula vya mifugo (Madini) kwa Mkurugenzi wa Kiwanda cha Input Agri Farmers LTV kinachojihusisha na utengenezaji wa virutubisho hivyo Bw. Anzamen Muro (kulia) muda mfupi baada ya kufika kiwandani kwake kata ya Tarate Mei 29, 2023 ikiwa ni sehemu ya operesheni ya ukaguzi kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo iliyofanywa kwa muda wa siku tatu (3) na TVLA kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Mkoa wa Arusha Mei 29 hadi 31, 2024
Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo (kushoto) akipata maelezo kuhusu utotoleshaji na utunzaji wa wadudu wanaotumika kuongeza protini kwa Mifugo na Samaki (Inzi Chuma) kutoka kwa mtaalamu wa utunzaji wa wadudu hao wa Kampuni ya Chanzi Bw. Deogratius Mulokozi (kulia) kata ya Temi (Njiro Viwandani) Mei 29, 2024 ikiwa ni sehemu ya operesheni ya ukaguzi kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo iliyofanywa kwa muda wa siku tatu (3) na TVLA kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Mkoa wa Arusha Mei 29 hadi 31, 2024.
Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo (mbele kushoto) akitoa elimu kuhusiana na umuhimu wa upimaji wa vyakula vya mifugo kwa mzalishaji wa vyakula vya hivyo kutoka kiwanda cha Pokea Investment LTD Dkt. Kastuli Sarwat muda mfupi baada ya kufika kiwandani kwake kata ya Oltrumet Mei 30, 2023 ikiwa ni sehemu ya operesheni ya ukaguzi kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo iliyofanywa kwa muda wa siku tatu (3) na TVLA kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Mkoa wa Arusha Mei 29 hadi 31, 2024
Mfugaji wa kuku wa Nyama na Mayai Bi. Veronica Mally (kushoto) kutoka kata ya Engutoto Njiro akielezea utaratibu anaoutumia kupata vyakula vya Mifugo vilivyohakikiwa ubora kwa Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo (katikati) na Mtaalam wa Mifugo kutoka Idara ya Malisho na Rasilimali za vyakula vya Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Theodata Sallema (kulia) Mei 31, 2023 ikiwa ni sehemu ya operesheni ya ukaguzi kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo iliyofanywa kwa muda wa siku tatu (3) na TVLA kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Mkoa wa Arusha Mei 29 hadi 31, 2024.
Mtaalam wa Mifugo kutoka Idara ya Malisho na Rasilimali za vyakula vya Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Theodata Sallema (wa pili kushoto) akitoa elimu pamoja na kufanya usajili wa Kampuni kwenye mfumo wa Wizara wa kutoa vibari wa MIMIS ili waweze kupata cheti cha kufanya biashara kwa Meneja wa Uthibiti Ubora wa Kampuni ya Farm Access LTD inayojishughulisha na uzalishaji wa pembejeo za Mifugo Bw. Abubakari Hajji (katikati) alipotembelewa kiwandani Oltrumet Mei 29, 2024 ikiwa ni sehemu ya operesheni ya ukaguzi kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo iliyofanywa kwa muda wa siku tatu (3) na TVLA kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Mkoa wa Arusha Mei 29 hadi 31, 2024
Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo (wa tatu kutoka kushoto) akipata maelezo  kutoka kwa Mfugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Bw. Charles Kibwana wa kata ya Lemara kuhusiana na utaratibu anaoutumia kupata vyakula vya Mifugo vilivyohakikiwa ubora Mei 31, 2023 ikiwa ni sehemu ya operesheni ya ukaguzi kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo iliyofanywa kwa muda wa siku tatu (3) na TVLA kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Mkoa wa Arusha Mei 29 hadi 31, 2024
Mtaalam wa Mifugo kutoka Idara ya Malisho na Rasilimali za vyakula vya Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Theodata Sallema (wa pili kushoto) akitoa Elimu ya umuhimu wa uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo kwa muuzaji wa vyakula vya Mifugo Bw. Mussa Kaniki alipotembelewa dukani kwake kata ya Unga Limited Mei 31, 2024 ikiwa ni sehemu ya operesheni ya ukaguzi kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo iliyofanywa kwa muda wa siku tatu (3) na TVLA kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Mkoa wa Arusha Mei 29 hadi 31, 2024

Post a Comment

0 Comments