Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amefanya kikao na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe tarehe 14 Agosti, 2024.
Kikao hicho kilichofanyika pembezoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kimejadili juu ya utekelezaji wa majukumu ya kidiplomasia yanayoendelea kutekelezwa na watumishi wa ubalozi huo.
“ Serikali ina imani nanyi ndio maana ikawaleta kutekeleza majukumu katika kituo hiki, hivyo, ni vema mkajituma na kufanya kazi kwa tija ili kuweza kuleta matokeo makubwa kwa maslahi ya Taifa letu” alisema Waziri Kombo.
Pia, ameeleza kuwa Wizara inahitaji kuona Balozi za Tanzania nje zinatekeleza diplomasia ya uchumi kwa vitendo na kuwasilisha taarifa zenye matokeo hususan katika sekta za biashara, uwekezaji, na utalii.
Aidha, Waziri Kombo ametembelea miradi mbalimbali ya maendeleo yenye umiliki wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zimbabwe ikiwemo, nyumba za makazi za watumishi wa Ubalozi, nyumba za makazi za kibiashara, jengo la ofisi la ubalozi na kiwanja cha ubalozi huo chenye ukubwa wa ekari saba (7).
Waziri Kombo amemueleza Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe kuwa ziara yake katika miradi hiyo imekuwa ya mafanikio kwa kuwa amejionea namna Ubalozi unavyojituma katika kutekeleza majukumu yake pamoja na jitihada za kukuza ushirikiano na nchi hiyo rafiki.
Vilevile, miradi hiyo kwa upande mwingine imeuwezesha ubalozi kupata nyumba kwa ajili ya watumishi wake na hivyo kuipunguzia Serikali gharama ya kupangisha nyumba na za uendeshaji kwa ujumla.
Hivyo, Waziri Kombo amesisitiza kuwa miongoni mwa masuala ambayo atayatilia mkazo katika utekelezaji majukumu yake ni pamoja na kuona Balozi za Tanzania nje zinaendeshwa kwa tija ili kuongeza pato la taifa.
Waziri Kombo akitembelea miradi ya maendeleo katika Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
0 Comments