Ticker

6/recent/ticker-posts

‘’NAKWENDA KUTAFUTA BILIONI 3.6 NIZILETE ILI VIVUKO VIKAMILISHWE’’ RAIS SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kupeleka Shilingi Bilioni 3.6 ambazo mkandarasi anazidai ili aweze kukamilisha ujenzi wa vivuko vipya vinavyoendelea kujengwa Mkoani Mwanza pamoja na Mkoani Dar es Salaam.

Rais Samia ametoa ahadi hiyo Tarehe 14 Oktoba, 2024 alipokuwa akizungumza na Wananchi wakati wa maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, sherehe zilizofanyika Kitaifa katika uwanja wa CCM Kirumba Mkoani Mwanza.

Akizungumza kuhusu miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na Serikali Mkoani Mwanza ikiwemo miradi ya maji, ujenzi wa barabara na miundombinu yake, ujenzi wa jengo la abiria uwanja wa ndege Mwanza pamoja na miradi mingine mikubwa ikiwemo ujenzi wa Daraja la JPM linalokwenda kuunganisha Wilaya za Misungwi na Sengerema, Rais Samia amesema Serikali itahakikisha miradi yote inatekekelezwa na kumalizwa kwa wakati ili iweze kutumiwa na Wananchi katika kuwaletea maendeleo.

‘’Kuhusu suala la vivuko, nilipoingia Mwanza nilifuatilia ujenzi wa vivuko na nikaambiwa ujenzi umefikia mbali sana, kunatakiwa fedha Bilioni 3.6 ili vivuko vile viweze kukamilishwa, nataka niwaahidi wana Mwanza, nakwenda kutafuta Bilioni 3.6 nizilete ili vivuko vikamilishwe na viweze kufanya kazi.’’ Amesema Rais Samia.

Katika mwaka huu wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) inaendelea na ujenzi wa jumla ya vivuko vitano vipya vitakavyokwenda kutoa huduma katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza ikiwemo kivuko kitakachokwenda kutoa huduma maeneo ya Ijinga na Kahangala Wilayani Magu, Bwiro na Bukondo Wilayani Ukerewe, Nyakaliro na Kome na Buyagu na Mbalika Wilayani Sengerema pamoja na Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza. Ujenzi wa vivuko hivyo kwa wastani, umefikia zaidi ya asilimia 85%.

Maeneo mengine ambako Serikali inaendelea na ujenzi wa vivuko vipya ni pamoja na eneo la Mafia na Nyamisati Mkoani Pwani ambako tayari ujenzi wa kivuko kipya kitakachokwenda kutoa huduma eneo hilo umekwishaanza na umefikia zaidi ya asilimia 35% za ujenzi wake. Eneo jingine ni Magogoni Kigamboni ambako Serikali inatarajiwa kupeleka vivuko vidogo viwili (Sea Taxi Ferries) kwa ajili ya kurahisisha huduma za usafiri eneo hilo.

Post a Comment

0 Comments