Ticker

6/recent/ticker-posts

RC Chalamila Apongeza Ushirikiano wa TANESCO na Serikali za Mitaa


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, leo amefungua kikao kazi maalum kilichoandaliwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ajili ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kutoka Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ubungo. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mhe. Chalamila amesema kuwa Serikali za Mitaa, kupitia viongozi wake, ni wadau muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini, hasa miradi ya nishati ambayo mingi hutekelezwa katika ngazi ya mitaa.

“Wenyeviti wa mitaa ni kiungo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya TANESCO kwa sababu miradi hiyo inatekelezwa katika maeneo yao. Ni imani yangu kuwa kupitia kikao hiki, viongozi wetu wa mitaa watakuwa mabalozi wazuri wa huduma zinazotolewa na TANESCO na pia watashiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu ya shirika,” alisema Mhe. Chalamila.

Aidha, alilipongeza Shirika la TANESCO kwa kutambua umuhimu wa kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za uhakika. Alisisitiza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu kuelekea mafanikio ya pamoja katika sekta ya nishati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, alisema kuwa shirika hilo limeamua kuandaa kikao kazi hicho kwa lengo la kujenga mfumo thabiti wa mawasiliano kati ya TANESCO na viongozi wa mitaa, sambamba na kuwaelimisha kuhusu shughuli na huduma zinazotolewa na shirika hilo.

“Tunataka viongozi hawa wawe sehemu ya TANESCO kwa kuwa ni wao wanaoishi karibu na wananchi. Kupitia mawasiliano ya moja kwa moja, tunaweza kufahamu changamoto na maoni ya wananchi kuhusu huduma zetu, na kwa pamoja kuboresha huduma hizo,” alieleza Bw. Twange.

Katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, Bw. Twange alikabidhi majiko ya umeme yenye matumizi madogo ya nishati kwa Mhe. Chalamila pamoja na baadhi ya viongozi wa mitaa waliohudhuria kikao hicho, ikiwa ni sehemu ya kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati salama na rafiki kwa mazingira.

Post a Comment

0 Comments