Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima amewahimiza wanawake watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Akizungumza Machi 4, 2026 katika kongamano la wanawake wa TANESCO, Dk. Gwajima amesema shirika hilo lina mchango mkubwa katika maendeleo endelevu ya taifa na ustawi wa wanawake kupitia upatikanaji wa umeme unaorahisisha maisha na kuinua uchumi wa familia.
Amesema ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ya kitaifa na inahitaji ushiriki wa sekta zote, ikiwemo wanawake wa TANESCO, ili kufanikisha mabadiliko yanayolengwa.
“Bila umeme wa uhakika katika kaya nyingi, mwanamke ataendelea kubeba mzigo wa kutumia kuni na mkaa, hali inayohatarisha afya na kupoteza muda wa kushiriki shughuli za maendeleo,” amesema.
Akirejea takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Dk. Gwajima amesema asilimia 81 ya kaya nchini bado zinatumia kuni na mkaa kupikia, ambapo asilimia 55 hutumia kuni na asilimia 26 mkaa. Ameeleza kuwa hali hiyo ni changamoto kubwa inayohitaji mapinduzi ya fikra na utekelezaji wa mikakati madhubuti.
Ameongeza kuwa matumizi ya umeme kwa kupikia bado ni madogo, yakifikia takribani asilimia 4.3 tu, huku gesi ikitumiwa na asilimia 9.4 ya kaya. Hivyo, ameitaka TANESCO kushirikiana na wizara yake pamoja na wadau wengine kubadili takwimu hizo kabla ya mwaka 2034.
Aidha, amemkumbusha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwamba tayari alizindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kufikisha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Dk. Gwajima pia ameeleza kuwa zipo dhana potofu kuwa kupikia kwa umeme ni gharama kubwa, ilhali teknolojia ya sasa imeleta majiko yanayotumia umeme kidogo kwa gharama nafuu.
Katika hatua nyingine, amesema wizara yake itashirikiana na maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata na vijiji kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya umeme kupikia, kwa lengo la kubadili mitazamo hasi na kuhamasisha jamii kukumbatia mabadiliko hayo.



0 Comments