
Na Alex Sonna, Dodoma
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amewataka watumishi wa umma nchini kuhakikisha wanazingatia wajibu na mamlaka waliyopewa katika kutoa huduma bora kwa wananchi kwa misingi ya uadilifu, ili kufanikisha lengo kuu la Serikali la kuboresha utoaji huduma kwa umma.
Akizungumza leo Oktoba 9,2025 jijini Dodoma wakati akitoa tamko kwa waandishi wa habari katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Mkomi amesema Serikali inaendelea kujenga utamaduni wa kuheshimu mteja kama sehemu muhimu ya mageuzi ya kiutendaji serikalini.
Aidha, amezielekeza taasisi za umma kutumia wiki hiyo kama fursa ya kujitafakari, kujifunza na kujipima kupitia mrejesho wa wateja wao, ili kuboresha tabia, mienendo na taratibu za utoaji huduma kwa manufaa ya taifa.
“Kwa mantiki hiyo, ninawaelekeza watumishi wote wa umma katika Wiki hii ya Huduma kwa Wateja kuzingatia wajibu na mamlaka waliyopewa kwa mujibu wa Katiba, kuhakikisha wanatekeleza jukumu la utoaji huduma bora kwa misingi ya uadilifu, ili kufikia lengo kuu la Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1)(b) ya Katiba, ambalo ni kuleta ustawi wa wananchi,” amesema Mkomi.
Amesisitiza kuwa utoaji wa huduma bora kwa kuzingatia misingi ya maadili utachangia kupunguza malalamiko, kuimarisha ustawi wa jamii na kujenga imani ya wananchi kwa Serikali yao.
Aidha, Mkomi amewakumbusha watumishi wote wa umma kuwa ustawi wa wananchi unapatikana kupitia utoaji wa huduma bora unaozingatia maadili ya utendaji na taaluma zao.
Amesema ni muhimu watumishi wa umma kuwa nadhifu, waaminifu, wakarimu, wenye heshima, wanaojali utu, wanaoepuka rushwa na wanaowaheshimu wananchi wanaowahudumia.
Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha taasisi za umma na binafsi kuboresha huduma wanazotoa, kuongeza uwajibikaji, na kujenga utamaduni wa kuheshimu mteja kama sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa.
Hata hivyo , Mkomi ametumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa umma kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu, akisisitiza kuwa ni haki ya kikatiba ambayo kila mtumishi anapaswa kuitumia ipasavyo.
Amesema kushiriki katika uchaguzi ni njia mojawapo ya kuimarisha demokrasia na kuchagua viongozi watakaosimamia vyema masuala ya maendeleo na ustawi wa wananchi.

0 Comments