Ticker

6/recent/ticker-posts

BODABODA SHINYANGA WATOA TAMKO KUELEKEA SIKUKUU YA KRISMAS

Na William Bundala-Shinyanga

Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki za Biashara Mkoa wa Shinyanga (CHAMWAPITA) kimetoa tamko la kupinga na kukemea kauli za uchochezi zinazotolewa na wanaharakati wa mtandaoni zinazohamasisha vurugu nchini na kuwataka wanachama wa chama hicho kutotumika kuvuruga amani.

Tamko hilo limetolewa leo na Mwenyekiti wa chama hicho Idsam Mapande wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia tetesi za kuwepo kwa baadhi watu wanaochochea vurugu mitandaoni.

“Tunapinga na kukemea kauli za kichochezi zinatolewa na wanaharakati wa mtandaoni ambao wengi wao hawaishi nchini, ila wanatumika na wanasiasa waliopo hapa ambao lengo lao ni kuifanya nchi kukosa utulivu,Tunapenda kuwashauri kwamba kama wana nia ya dhati ya kujenga nchi, tunawashauri warudi nchini tujenge nchi kwa pamoja na sio kuwachochea vijana kufanya vurugu” Amesema Mapande.

Mapande ameongeza kuwa vurugu ambazo zilitokea Oktoba 29 zilileta athari kubwa kwa maafisa usafirishaji ikiwa ni Pamoja na kutikisika kiuchumi kwa wanachama wengi na kusababisha kuteteleka kwa baadhi ya familia zao.

“Itakumbukwa kwamba kwa Mkoa wa Shinyanga hasa Wilaya ya Kahama na kipekee Manispaa ya Kahama vurugu za wakati na baada ya uchaguzi zilileta athari za moja kwa moja kwetu kama Maafisa Usafirishaji kwa sababu shughuli zetu zinategemea amani na utulivu inayowafanya wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi ambapo ili wafike kwenye maeneo yao ya kazi hutumia kwa kiasi kikubwa usafiri wetu kuwasafirisha pamoja na mizigo yao” Ameongeza Mapande.

Katika hatua nyingine Mapande amesema kuwa kupitia chama chao,wameweka utaratibu wa kuwatambua watu ambao wanachochea vurugu wanaofika kwenye vijiwe vya bodaboda na kushawishi vurugu.

“Chama cha Wasafirishaji tumeweka utaratibu rasmi wa kuwatambua Bodaboda, Bajaji na Maguta ili iwe rahisi kuwabaini wale ambao sio wenzetu ambao hufika kwenye vituo vyetu vya kazi na kuleta taharuki na uchochezi” Amesisitiza Mapande.

Nao baadhi ya madereva pikipiki Godifrey Ashery na Shukuru Peter wamesema kuw wamejipanga vizuri kuhakikisha vitendo vya vurugu havitokei tena kwani vitendo hivyo vimeleta madhara makubwa kama kuharibika kwa barabara na kukosekana kwa nishati ya mafuta katika manispaa ya Kahama” Wamesema madereva hao.

Kwa mujibu wa Chama cha madereva na wamiliki wa pikipiki za biashara mkoa wa Shinyanga (CHAMWAPITA),mkoa una jumla ya pikipiki za magurudumu mawili zipatzo elfu 30,bajaji za mizigo 2000 na bajaji za abiria zikiwa ni 8000.

Post a Comment

0 Comments