Ticker

6/recent/ticker-posts

CCM YAFANYA MAZUNGUMZO NA MJUMBE MAALUM WA UMOJA WA MATAIFA MAKAO MAKUU YA DODOMA

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Ndg. Asha-Rose Migiro,leo tarehe 11 Machi 2026 amefanya mazungumzo jijini Dodoma na Balozi Parfait Onanga-Anyanga, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa iliyopo Addis Ababa (UNOAU).

Balozi Onanga-Anyanga yupo nchini Tanzania kwa nafasi yake kama Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe.António Guterres.

Kikao hicho ni sehemu ya mashauriano ya Mjumbe huyo na wadau mbalimbali wa kitaifa kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu mustakabali wa kisiasa kufuatia Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025, pamoja na juhudi pana za kuimarisha amani, demokrasia na mshikamano wa kitaifa nchini Tanzania.

Katika mazungumzo hayo, Ndg. Asha-Rose Migiro alisisitiza dhamira ya muda mrefu ya Tanzania katika kuendeleza utawala wa kidemokrasia, ushiriki wa kisiasa kwa njia ya amani na kuheshimu utawala wa sheria.

Alibainisha kuwa Tanzania inaendelea kuongozwa na misingi ya Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala Bora, pamoja na viwango vya kimataifa vilivyowekwa katika Tamko la kimataifa la Haki za Binadamu na Mkataba wa kimatifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa.

Katibu Mkuu pia alieleza kuhusu mageuzi ya kisheria katika Tume ya Uchaguzi na taasisi nyingine yaliyofanyika kwa lengo la kuimarisha mfumo wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sheria mpya za uchaguzi mwaka 2024 na hatua mbalimbali zilizolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi.

Mazungumzo hayo pia yaligusia matukio ya vurugu yaliyojitokeza katika baadhi ya maeneo nchini wakati na baada ya uchaguzi, ambayo yalisababisha upotevu wa maisha na uharibifu wa mali, ikiwemo mashambulizi dhidi ya ofisi za CCM. Ilibainishwa kuwa hatua stahiki zilichukuliwa kurejesha hali ya utulivu na amani nchini.

Pande zote mbili zilisisitiza umuhimu wa kuendelea kwa mazungumzo na maridhiano miongoni mwa wadau wa kitaifa. Hali kadhalika Katibu Mkuu wa CCM alimthibitishia Balozi Onanga-Anyanga kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano wake na jumuiya ya kimataifa katika kuimarisha amani, usalama na maendeleo jumuishi.

CCM imepongeza ushirikiano madhubuti uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Mataifa na kuthibitisha dhamira yake ya kustawisha umoja wa kitaifa, utulivu na demokrasia katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Post a Comment

0 Comments