Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MCHENGERWA AUONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA MKUTANO WA PILI WA DUNIA WA TIBA ASILI


Na John Mapepele, New Delhi

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa leo ameuongoza ujumbe wa Serikali ya Tanzania katika uzinduzi wa Mkutano wa pili wa dunia wa Tiba Asili unaoratibiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwenye ukumbi wa kimataifa wa Bharat Mandapam jijini New Delhi India.

Mhe. Mchengerwa amepongeza juhudi zinazofanywa na WHO za kuileta dunia pamoja ili kujadili suala la Tiba Asili na kupata ufumbuzi katika masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na utawala na udhibiti wa tiba asili, utafiti na ushahidi wa kisayansi, ujumuishaji wa tiba asili katika mifumo ya afya, matumizi endelevu ya raslimali za kiasili na uendelezaji wa raslimali watu kwenye eneo la Tiba Asili.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Mheshimiwa Prataprao Ganpatrao Jadhav, Waziri wa Nchi (Independent Charge), Wizara ya Tiba Asili (AYUSH), na Waziri wa Nchi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Familia ya Serikali ya India, mbele ya Mheshimiwa Jagat Prakash Nadda, Waziri wa Afya na Ustawi wa Familia wa Serikali ya India. Hafla hiyo imewakutanisha Mawaziri, watunga sera wakuu, na wadau wa sekta ya afya kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus akitoa hotuba yake kwa njia ya video kwenye ufunguzi huo amewasihi wajumbe wa mkutano huo kujadili kwa kina mada mbalimbali ili kubadilishana uzoefu na kwamba kwa sasa Tiba Asili bado itaendelea kuwa na mchango mkubwa kwa wanadamu kwa kuzingatia kuwa tiba asili ni sehemu ya tamaduni za watu katika mataifa yao.

Pembezoni mwa mkutano huo, Tanzania inatarajia kusaini Hati mbili za Makubaliano (MoU) na Serikali ya India kuhusu ushirikiano katika sekta ya afya na tiba asilia (Ayurveda), hatua itakayosaidia kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi, kuongeza uwezo wa rasilimali watu, na kuimarisha matumizi salama ya tiba asilia nchini.


Kusainiwa kwa hati hizi mbili za makubaliano ni hatua muhimu kwa Tanzania, kwani kutaimarisha ushirikiano wa kitaasisi na India katika maeneo ya kipaumbele ya sekta ya afya, kuongeza uwezo wa rasilimali watu wa sekta ya afya, kuimarisha udhibiti na matumizi salama ya tiba asilia, pamoja na kuchangia jitihada za Serikali katika kuimarisha mifumo ya huduma za afya na kufikia Bima ya Afya kwa Wote.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unaakisi dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kukuza tiba asilia salama, yenye ushahidi wa kisayansi na inayosimamiwa kwa misingi madhubuti ya udhibiti, sambamba na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu ya afya kwa watu wote.

Mkutano huo wa siku tatu unatarajiwa kufungwa na Desemba 19, 2025 na Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi, jambo linaloonesha uzito na umuhimu mkubwa wa mkutano huo katika ngazi ya juu ya kisera.





Post a Comment

0 Comments