Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI LONDO AIPONGEZA SIDO KWA KUTEKELEZA AGENDA YA SIKU 100 YA RAIS SAMIA

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo amelipongeza Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kutekeleza ahadi ya siku 100 ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni moja kwa wajasiriamali ili kuendeleza miradi mbalimbali ya viwanda nchini.

Amebainisha hayo Januari 23, 2026, alipofanya ziara ya kikazi katika shirika hilo na kuipongeza menejimenti kwa kasi ya kuridhisha ya utekelezaji wa maelekezo ya serikali.

Mhe. Londo amesisitiza kuwa viwanda vidogo ni moyo wa uchumi endelevu kwani vinamsaidia mwananchi hasa vijana kupata ajira na kuleta maendelwo kuanzia ngazi ya familia na kuchochea uingizaji wa fedha za kigeni.

Amesema kupitia SIDO, bidhaa za Kitanzania zinaweza kuteka soko kubwa la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), jambo litakaloinua hadhi ya viwanda vya ndani katika medani za kimataifa.

Kufuatia ziara hiyo, Naibu Waziri ameiagiza SIDO kuangalia namna ya kuongeza kutoa ruzuku (grants) kwa vijana ili kuhakikisha wanawekeza kwa kutumia rasilimali zilizopo bila kukwama, lengo ni kuhakikisha kuwa ukosefu wa mtaji haubaki kuwa kikwazo kwa vijana wabunifu wanaotaka kuingia katika sekta ya uzalishaji na viwanda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. Audax Bahweitima, amesema Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs) inalenga kuboresha miundombinu ya biashara na teknolojia na kusisitiza kuwa SIDO ndiye mtekelezaji mkuu wa sera hiyo kwa kuhakikisha upatikanaji wa fedha na zana za kisasa za uzalishaji unawafikia walengwa kwa wakati.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji, amesema kuwa hadi sasa wanufaika 196 wamefikiwa na mikopo hiyo, na kufanikiwa kuzalisha jumla ya ajira 546. Takwimu hizo zinaonyesha mafanikio makubwa kwa kundi la vijana, ambao wamechukua nafasi 436 kati ya ajira hizo mpya zilizotengenezwa.

Aidha, Prof. Mpanduji ameongeza kuwa kupitia ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM), wametoa ruzuku ya shilingi milioni 51 kwa vijana tisa ili kukuza viwanda vyao.

Post a Comment

0 Comments