Ticker

6/recent/ticker-posts

MASHINDANO YA LIGI YA MUUNGANO YAIMARISHA UNDUGU, UMOJA NA MSHIKAMANO KWA WATANZANIA

Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) imesema itaendelea kutumia tasnia ya sekta ya michezo ili kujenga mahusiano ya undugu, ujamaa, umoja na mshikamano wa Watanzania ili kuenzi misingi ya Muungano.

Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa (Januari 23, 2026) na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Richard Muyungi wakati wa ziara yake ya kutembelea kambi ya timu ya Netiboli ya Ofisi hiyo inayoshiriki mashindano ya Ligi ya Muungano wa netiboli inayoendelea katika Uwanja wa Amani Complex, Zanzibar.

Dkt. Muyungi amesema michezo ni sekta muhimu inayotumika katika kujenga mashirikiano na uhusiano katika jamii na hivyo Ofisi hiyo itaendeleza jitihada mbalimbali katika kuhakikisha michezo itakuwa sehemu muhimu katika kuimarisha Muungano.

“Nia na malengo ya waasisi wetu wakati wanaanzia Muungano ni Pamoja na kuhakikisha wanatumia fursa mbalimbali ikiwemo michezo ili kuweza kujenga mahusiano ya undugu, familia na fursa nyingine za kijamii na kiuchumi” amesema Dkt. Muyungi.

Ameeleza kuwa kupitia sekta ya michezo hususani mashindano ya Ligi ya Netiboli, Ofisi hiyo imeweza kutangaza vyema Muungano ambapo wachezaji wa timu wameweza kuwa kucheza kwa juhudi kubwa na kuibuka kwa matokeo ya ushindi katika michezo yake.

Aidha mbali na ziara hiyo Dkt. Muyungi pia alikabidhi zawadi ya pesa taslimu Shilingi 500,000/- kwa kila mchezaji wa timu hiyo ikiwa ni sehemu ya motisha kwa wachezaji hai ili kuwaongezea morali ya kupata matokeo ya ushindi katika michezo yake iliyosalia.

“Nimetoa zawadi hii ya pesa kama motisha kwenu kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi, niseme tu yajayo yanafurahisha…tuongeze juhudi katika michezo iliyosalia ili tuweze kuchukua ubngwa wa mashindano haya” amesema Dkt. Muyungi.

Kwa upande wake Kocha wa Timu wa hiyo, Mafuru Buriro amesema menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kwa kuiwezesha timu kupata mahitaji yote ya msingi hatua iliyowezesha kuwa na kambi nzuri iliyojiandaa vyema kwa ajili ya mashindano hayo.

“Tunamshukuru sana Katibu Mkuu kwa kuwa karibu na timu tangu mwanzo wa mashindano haya kwani hiyo ndiyo iliyokuwa siri ya mafanikio ya ushindi wat imu katika michezo yote tuliyocheza” amesema Buriro.

Amesema timu hiyo imecheza jumla ya michezo 10 ambapo imeshinda michezo 9 na kupoteza mchezo dhidi ya timu ya Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) amba oni mabingwa watetezi wa mashindano hayo.

Kwa upande Katibu wa Klabu ya Michezo Ofisi ya Makamu wa Rais, Marwa Nyaisawa amesema mashindano ya Ligi ya Muungano ya Netiboli ni moja ya mashindano mahsusi katika kuonesha umma kuwa Ofisi hiyo imejiandaa vyema kwa ajili ya kuonesha ushindani katika michezo mbalimbali.

Naye mchezaji wa timu hiyo, Bi. Habiba Mhina ameishukuru Menejimenti ya Ofisi hiyo kwa kutoa nafasi kwa watumishi wanawake kuweza kushiriki maonesho hayo kwani yameweza kwani mbali na kuimarisha afya michezo hiyo pia imeweza kuwakutanisha na wadau mbalimbali.

Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Netiboli mwaka 2026, yalishirikisha jumla 11 ikiwemo timu sita (06) kutoka Tanzania Bara na timu tano (05) kutoka Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments