Na Mwandishi Wetu
HOSPITALI ya Shifaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imezindua Idara ya mfumo wa upumuaji inayotumia teknolojia ya hali ya juu kwa magonjwa yanayohusu mfumo upumuaji ambayo ni ya kisasa zaidi kwa hapa nchini.
Uzinduzi wa Idara hiyo ulifanyika juzi jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali mashuhuri pamoja na viongozi wa serikali na wale wa sekta binafsi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kitengo hicho, Mkurugenzi Msaidizi magonjwa yasiyo ya kuambukiza Wizara ya Afya, Omari Ubuguyu, aliipongeza hospitali hiyo kwa kuanzisha Idara hiyo aliyosema inatumia teknolojia ya hali ya juu.
“Kwa aina ya teknolojia niliyonayo hapa na ujuzi wa hali ya juu utakaokuwa kwenye idara hii naona ni hatua kubwa sana kwenye sekta ya afya, nawapongeza sana viongozi wa Shifaa. Na uzuri ni kwamba situ kwamba itahusika na magonjwa ya mfumo wa upumuaji bali itashughulika pia na kinga ya magonjwa hayo,” alisema
Aidha, alisema idara hiyo ni muhimu sana kwa magonjwa ya mfumo wa kupumua kwa watu waliopata maambukizi kama ya kifua kikuu, maradhi ya COVID 19 na magonjwa mengine ambayo yanaathiri kifua.
“Katika ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi yaani PPP wenzetu Shifaa kwa kuanzisha kitengo hiki wamefanya jambo zuri sana kwasababu wanasaidia jitihada za serikali kusogeza huduma karibu kwa wananchi,” alisema Ubuguyu
Naye Dk Mwanaada Kilima ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji wa hospitali ya Shifaa, alisema idara hiyo itahusika na kinga na tiba ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji.
Aidha, alisema kwenye idara hiyo wagonjwa watakuwa wakipimwa maradhi ya kifua na pumzi na radiolojia na kuongeza kuwa kitengo hicho cha kipekee kimeongeza thamani ya matibabu ya aina hiyo kwa watanzania wote.
“Tunajivunia kuwa na idara kama hii hapa nchini kwasababu mtu akiugua moyo anajua aende wapi kutibiwa moyo akiugua mifupa anajua pakwenda na sasa mtu akiugua mfumo wa upumuaji atajua aende Shifaa ndiko atapata suluhusisho la matatizo yake,” alisema
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Bashir Haroon alisema hospitali ya Shifaa imejitahidi kuweka madaktari na wataalamu wabobezi kwenye taaluma za kitabibu ili wawahudumie watanzania.
“Nawashukuru sana watu wote ambao wamekuwa nasisi mpaka kufika hapa na kufanikiwa kuanzisha Idara hii ya mfumo wa upumuaji tunaomba serikali iendelee kutuunga mkono ili tuweze kuwahudumia watanzania wenzetu,” alisema
Alisema uzinduzi wa idara hiyo ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za afya kwa wananchi na kukabiliana na ongezeko la magonjwa yanayoathiri mapafu na njia za hewa.
Alisema kuanzishwa kwa idara hiyo kutasaidia kuboresha utambuzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali ya mfumo wa upumuaji yakiwemo pumu, maambukizi ya mapafu, kifua kikuu na magonjwa mengine yanayohusiana na upumuaji.
Aidha, alisema kitengo hicho kimewekewa vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu pamoja na wataalamu waliobobea katika magonjwa ya mfumo wa upumuaji ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na kwa wakati.
Alisema lengo la kuanzisha kitengo hicho ni kupunguza adha ya wagonjwa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma maalum za matibabu ya mapafu na njia za hewa, huku pia kikitarajiwa kusaidia kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya mfumo wa upumuaji.






0 Comments