Ticker

6/recent/ticker-posts

JUKWAA LA WAHARIRI WAIPONGEZA REA UTEKELEZAJI MIRADI YA NISHATI YA UMEME VIJIJINI, USAMBAZAJI GESI ASILIA

Na Said Mwishehe,

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa pongezi kwa Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini(REA) kwa kazi kubwa na nzuri ya kusambaza nishati ya umeme katika maeneo ya vijijini kote nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) leo Machi 8,2026 baada ya Wahariri kufanya ziara ya kikazi kutembelea mradi uliofadhiliwa na REA wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia kwenye nyumba na makazi mkoani Pwani.

Mradi huo umetekelezwa katika mikoa ya Mtwara ,Lindi na Pwani katika eneo la Kisevule ambapo jumla ya fedha ambazo zimetolewa na REA kufadhili mradi huo ni Sh.Bilioni 6.8 na aliyepewa jukumu la ujenzi wa miundombinu ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC).Wananchi waliofungiwa gesi hiyo kwa sasa wanafurahia maisha kwani Sh.1000 inatosha kuweka gesi inayoweza kupika kwa siku tatu .Wenyewe wanainjoi tu kwa sasa.

“Wahariri leo wamepata nafasi ya kutembelea mradi wa kusambaza gesi asilia majumbani kwa ajili ya kupata nishati safi ya kupikia ambapo REA wameufadhili mradi huu na kutekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania)TPDC).

“Wakati REA inaanza kuna watu walitaka kupinga lakini sasa hivi imekuja kuonekana kwamba kwa kweli ni mkombozi halisi katika maendeleo ya Tanzania kwa maana ukienda vijijini sehemu yoyote umeme umefika.

“Zamanı ilikuwa tukisafiri ukifika mahali fulani ukaona taa za umeme unajua tumefika mjini lakini sasa hivi kama unakwenda na dhana hiyo utapotea sana kwa sababu karibu kila kijiji kina umeme na hii kazi imefanya na REA,”amesema Balile.

Amefafanua kuwa mbali na kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania pia yeye ni Mwenyekiti wa Afrika Mashariki na amekuwa akienda nchi mbali mbali na wanakwenda vijijini.“Moja ya swali ambalo naulizwa Tanzania mmewezaje kufikisha umeme jijini.”

Akieleza zaidi amesema kasi ya REA katika kusambaza umeme vijijini imefika hatua ambao wakati mtu anajenga nyumba akiwa katika hatua ya msingi tayari REA wameshafikisha nguzo kuweka umeme.

“Kwahiyo katika hali hiyo Tanzania tumepiga hatua kubwa sana mradi kama huu ambao umefadhiliwa na REA unaonyesha jinsi gani sasa tunavyoweza sisi wenyewe watanzania kujenga nchi yetu wenyewe kwani hili suala la misaada misaada tulipunguze maana wanatupa misaada wanatupa na masharti.

“Lakini Wahariri wameshuhudia tumeanza hapa na hii ziara itaendelea tutakwenda kushuhudia na maeneo mengine lakini uhalisia REA wanafanya kazi nzuri na wanastahili pongezi.Mimi ni moja ya wanufaika wa REA kule Bukoba niliomba umeme jana na kesho yake saa 11 jioni umeme ukawaka pale nyumbani.”

Kuhusu mradi wa kusambaza gesi asilia majumbani na katika taasisi ,Balile amesema nishati hiyo inakwenda kumkomboa mwananchi “Gesi asili nayo imeanza kusambazwa na najua baadhi ya watu wametumia sana mkaa na kuni…

“Na wanadhani kwamba ndio kitu kinachoivisha chakula lakini kadri tunavyoendelea ni wazi watu wengi wameacha kutumia mkaa ambao gharama zake ziko juu ukilinganisha na bei ya gesi ya kupikia.REA mnafanya kazi nzuri sana.”

Post a Comment

0 Comments