Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA KUKAMILIKA KWA JENGO LA TEHAMA CoICT UDSM

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeridhishwa na kukamilika kwa jengo jipya la TEHAMA katika Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CoICT) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ikisema mradi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa Tanzania katika teknolojia zinazoibukia.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Husna Sekiboko, ilitembelea leo Machi 16, 2026 kituo hicho kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi huo na kuthibitisha kuwa ujenzi wa jengo hilo umekamilika. Vifaa muhimu kwa ajili ya kituo hicho tayari vimewasili na vinasubiri kufungwa kabla ya kuanza kwa shughuli za ufundishaji na utafiti.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Sekiboko amesema Akili Unde ni moja ya mapinduzi makubwa ya kiteknolojia katika dunia ya sasa, hivyo Tanzania inapaswa kujipanga kutumia fursa zinazotokana na teknolojia hiyo huku ikikabiliana na changamoto zake.

“Mapinduzi ya teknolojia katika kompyuta ni makubwa sana na yataendelea kwa miaka mingi. Baadhi ya kazi zinazofanywa na binadamu kwa sasa zinaweza baadaye kufanywa na kompyuta,” amesema.

Ameongeza kuwa miradi inayotekelezwa na vyuo vikuu mbalimbali nchini inaonesha matumizi mazuri ya fedha za umma na ina uwezo mkubwa wa kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

“Miradi tuliyoitembelea inaonesha wazi kuwa rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na zinaweza kuleta manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema serikali imejipanga kuongeza wataalamu katika eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Akili Unde kwa kusomesha Watanzania nje ya nchi, sambamba na kuimarisha miundombinu na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia.

Amesema kupitia mpango wa Samia Scholarship, serikali tayari imepeleka wanafunzi katika vyuo vikuu mahiri nchini Afrika Kusini na Ireland kusoma masomo ya Akili Unde, Sayansi ya Data na Sayansi Shirikishi.

“Pamoja na kupeleka wanafunzi kusoma nje ya nchi, tuna chuo cha Indian Institute of Technology Zanzibar ambapo tunapeleka wanafunzi wa eneo hilo katika ngazi ya uzamili,” amesema Prof. Mkenda.

Aidha, amewataka vijana kuona fursa kubwa zinazokuja kupitia maendeleo ya teknolojia, ambazo zinaweza kufungua milango ya ajira na ubunifu, huku akisisitiza matumizi sahihi na salama ya teknolojia hizo.

Akizungumzia ujenzi wa miundombinu unaofanywa na serikali katika ndaki hiyo, amesema utakapokamilika utaongeza udahili wa wanafunzi wapatao 351, huku pia ukiwa umechangia kutoa ajira 529 zikiwemo za kitaaluma na za muda mfupi.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, amesema kituo hicho kipya cha AI kitaiweka UDSM katika nafasi ya kuwa kitovu muhimu cha mafunzo na utafiti wa teknolojia za kisasa katika ukanda huu.

Amesema jengo hilo litasaidia kuendeleza utafiti wa kisasa katika Akili Unde, Sayansi ya Data na ubunifu wa kidijitali, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya chuo kikuu, sekta ya viwanda na taasisi za kimataifa za utafiti.

Post a Comment

0 Comments