Ticker

6/recent/ticker-posts

KUPIKA KWA GESI YA REA NI MWENDO WA BUKU TU “KILA NIKIPIKA NAMTAJA SAMIA”

Na Said Mwishehe, Pwani

MAISHA yamekuwa rahisi sana huku kwetu! Hivyo ndivyo anavyoanza kuelezea Mkazi wa Kisevule Center katika Kata ya Vikindu mkoani Pwani Mariam Mohamed ambaye kwa sasa anapika chakula kwa gesi asilia iliyofungwa nyumbani kwake kwa ufadhili wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

REA imetoa Kiasi cha fedha Sh.bilioni 6.8 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia ikiwemo ujenzi wa bomba kutoa gesi Mtwara hadi Pwani na kisha kupeleka gesi hiyo kwa kaya 1000 ikiwemo kaya ya Mariam mjane wa watoto watano.

Wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari walioko katika ziara iliyoandaliwa na REA kwa ajili ya kuangalia mradi huo wa usambazaji gesi asilia kwa wananchi wa Kisuvule wilayani Mkuranga mkoani Pwani ,Mkazi huyo amesema tangu aanze kutumia gesi ya REA maisha kwake yamekuwa marahisi sana hasa katika kuandaa mlo wa familia yake.

“Nashukuru sana kwani mradi huu umetusaidia sana yaani umetuokoa na hasa huu mwezi huu wa Ramadhani… kuna wepesi nauona kwanza nalala mapema na tunapika vyakula kwa wakati

“Namshukuru sana Mungu ,namshukuru sana mama yetu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwani katuokoa sana sana yaani kila nikipika siachi kumtaja Mama Samia kwa kutuletea gesi hii bure majumbani kwetu.”

Ameendelea kueleza kuwa kwa sasa hana wasawasi anapotaka kupika kwani hata gesi ikiisha ananunua kwa Sh.1000 tu na kuendelea na mapishi hivyo maisha yamekuwa rahisi .

“Siku za nyuma nilikuwa napika daku nahangaika lakini sasa hivi naweza kwanza kufanya shughuli zangu kisha nikalala na ikifika saa saba nikaamka nawasha gesi naandaa chakula changu na saa nane nakula maisha yanaenda.Kwa kusema mkweli maisha yamekuwa mepesi sana.”

Aidha amesema wakati mradi huo unataka kuanza baadhi ya wananchi hawakuwa tayari kuwekewa gesi hiyo katika nyumba zao kwa madai nyumba zitalipuka kwa gesi lakini kwa sasa wananchi hao wameanza kuomba namba za simu za REA ili wafungiwe mfumo huo wa gesi asilia unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

“Kwangu walivyokuja nikawaambia niko tayari kwani niliamini Rais wetu hawezi kuleta kitu kibaya kwa raia wake au wananchi wake lazıma ataleta kitu cha kutuokoa.”

Akiendelea kuelezea gesi hiyo iliyofungwa nyumbani kwake anasema hivi sasa hata watoto wake wanakimbilia jikoni kupika wakati alipokuwa akitumia mkaa walikuwa hawataki kupika.

“Tumewekewa gesi hii bure kabisa na ukweli Mwenyezi Mungu amjalie Mama Samia yaani ampe maisha marefu apate kuwasaidia wengine,”amesema Mariam na kusisitiza akinunua gesi ya Sh.1000 anapika kwa siku tatu.

Kwa upande wake Hussein Shemndolwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitangwi katika kijiii cha Kisimvule kata ya vikindu wilayani Mkuranga amesema wanaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia kwa kuwapatia mradi huo kwani wananchi wanafaidika na mradi huo.

“Kwasababu viwango ambavyo vinatumika kwa siku kama walivyosema ni Sh. 1, 000 kwa siku na wananchi ambao wameingiziwa huduma hiyo wamekuwa ni mashahidi.Hata hivyo nitoe ombi kwa REA na TPDC kuhakikisha mradi huu unakwenda katika nyumba nyingi zaidi ,tunazo Kaya 12000 hapa kwetu hivyo tunauhitaji mradi huu sana.”

Awali Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Mradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yessaya amesema Wakala huo ulitenga fedha kwa ajili ya kufadhili mradi wa usambazaji wa gesi asilia kupitia Mfuko wa REF ambapo takribani kaya 1000 na taasisi moja zimenufaika kwa kusambaziwa miundombinu ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia majumbani katika mkoa wa Lindi na Pwani.

“Mradi huo ni wa kimkakati kwa ajili ya kupunguza gharama za nishati ya kupikia, kulinda afya za wananchi na kupunguza athari za kimazingira zitokanazo na ukataji wa misitu kwa ajili ya nishati ya kupikia kwa wananchi wanaoishi Vijijini na kwenye vijiji miji.”

Kwa upande wake Mhandisi wa mradi huo kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mha. Anthony Karomba, amesema mradi huo wa kuunganisha wateja wa majumbani kwenye mtandao wa gesi asilia umegharamikiwa kwa fedha nyingi na Serikali kupitia REA na hivyo amewasihi wananchi kuendelea kuilinda miundombinu hiyo.

Post a Comment

0 Comments