Na Rose Ngunangwa, Iringa
Wanawake Mkoani Iringa wameaswa kuachana na mikopo almarufu kama Shikilia Dera au Ndala mkononi kwani mikopo hiyo imekuwa ikisababisha mali za familia kuuzwa au kutaifishwa ili kufidia na kuiacha familia ikiingia kwenye lindi la umaskini.
Mikopo hiyo imepewa jina la shikilia dera au kandamili mkononi kutokana na wanawake wanaochukua kulazimika kushikilia mavazi hayo au kandambili na kukimbia pale wanaposhindwa kupata rejesho kutokana na riba kubwa zinazotozwa.
Wito huu ulitolewa mjini Mafinga mwishoni mwa wiki wakati wa mdahalo ulioandaliwa na SOS Children’s Villages Iringa ili kujadili hali ya ukatili wa kijinsia wilayani humo, visababishi na namna ya kutokomeza vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, mkopaji anaweza akakopa shillingi laki moja ambapo hutakiwa kurejesha shilingi 150,000/- ndani ya mwezi mmoja kiwango ambacho wakati mwingine huwa kikubwa mno kwa mhusika huku riba ikipanda.
Akichangia hoja hiyo, Neema Kihongosi alisema kuwa uchukuaji holela wa mikopo hiyo ambayo pia huitwa Vimangala kwa upande wa akina mama umefanya watoto wengi wilayani humo kukosa huduma za msingi na matunzo kwani akina mama hao hutumia muda mwingi kufanya biashara ili waweze kupata marejesho na kushindwa kutimiza majukumu ya nyumbani.
“Watoto wengi wanataabika kutokana na ulevi kwani baadhi ya akina mama hushinda kwenye biashara kutwa wakitafuta marejesho na wanapotoka huko hupitia kwenye vilabu kunywa pombe na kurudi wamelewa bila kujali kama watoto wamekula, wameoga au la,” alisema Kihongosi.
Akichangia hoja hiyo, Steven Mponzi mkazi wa Nyororo amekiri kuwa mikopo hiyo huleta shida kubwa kwenye familia kwani akina mama wengi wamekuwa wakichukua bila kushirikisha waume zao ambapo muda wa marejesho ndipo hujua kwani wahusika huja kuchukua vitu vya nyumbani.
“Wakati mwingine mhusika hukimbia na kuachwa nyumba zikiuzwa na hivyo kuleta shida kubwa na msongo wa mawazo,” alisema Mponzi.
Wadau hao wameshauri sheria itungwe na kulazimisha mke au mume kutochukua mkopo bila uwepo wa mwenza wake ili kuokoa familia.
Mkoa wa Iringa unakabiliwa na changamoto kubwa ya ukatili huku wanaume wakilalamikia wanawake kuchukua mikopo mingi, kulewa kupita kiasi, wakati mwingine kuwapiga na hata kutelekeza familia.






0 Comments