Ticker

6/recent/ticker-posts

TBS ,FCC wakutana na wadau wa Pombe kutatua changamoto bidhaa hafifu na bandia

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani (FCC) wamekutana na wadau wa bidhaa za pombe nchini kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya matakwa ya sheria, kanuni na viwango vinavyosimamia sekta hiyo.

Kikao hicho kilichofanyika leo Machi 27, 2026 jijini Dar es Salaam, pia kimelenga kujadiliana na kubaini changamoto zinazowakabili wadau katika kukidhi matakwa ya kisheria pamoja na masuala ya ushindani, ili kupata ufumbuzi wake.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Mhandisi Yona Afrika, amesema kumekuwa na malalamiko yanayopokelewa na taasisi hizo kuhusu uwepo wa pombe duni na bandia katika soko, hali inayochangiwa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu.

“Bidhaa hizi zisipozingatia matakwa yaliyowekwa, zinaweza kuhatarisha afya na usalama wa walaji,” amesema Afrika.

Ameongeza kuwa TBS kwa kushirikiana na FCC zitaendelea kuimarisha usimamizi wa viwango ili kudhibiti ubora wa bidhaa pamoja na kuhakikisha ushindani wa haki katika soko.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi.Roberta Feruzi, amesema uwepo wa pombe duni na bandia si tu unaharibu ushindani wa haki bali pia husababisha malalamiko kutoka kwa walaji kuhusu thamani ya fedha wanazolipa na athari za kiafya.

Amebainisha kuwa hali hiyo pia hudhoofisha biashara halali na kuvuruga mazingira ya ushindani sawa kwa wafanyabiashara wanaofuata sheria.


Post a Comment

0 Comments