Msimamizi wa Bohari ya kuhifadhia mafuta (Depot) ya kampuni ya MOIL Energies, Sajad Habib Rai, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa huduma kwa saa 24 katika maeneo ya bohari, akisema hatua hiyo itaongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Sajad amesema kuwa utaratibu huo mpya unarahisisha shughuli za biashara na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma, hali itakayosaidia kupunguza ucheleweshaji wa mizigo ya mafuta.
Akizungumzia upatikanaji wa mafuta, amebainisha kuwa kampuni ya MOIL Energies ina akiba ya kutosha ya mafuta huku wakisubiri meli nyingine ambazo tayari zimetia nanga ili kushusha bidhaa hiyo.
Ametoa kauli hiyo baada ya ziara ya Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, aliyetembelea bohari hiyo iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Sajad amesema kuongezeka kwa muda wa kazi kwa watumishi wa TRA kutasaidia kuongeza ufanisi zaidi katika shughuli za biashara, jambo ambalo wamepokea kwa mikono miwili.
“Tunampongeza Kamishna Mwenda kwa utendaji wake. Kwa sasa TRA inatoa ushirikiano mkubwa kwa wafanyabiashara, na tunaona maboresho kila siku, hali inayotuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema Sajad.
Aidha, ameunga mkono utaratibu mpya wa uuzaji wa mafuta ya dizeli na petroli uliowekwa na TRA, akisema umeondoa changamoto ya uchepushaji wa mafuta na kuhakikisha kila mzigo unafika mahali ulipokusudiwa.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, amesema mamlaka hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha huduma zinatolewa kwa saa 24 katika bohari zote za mafuta nchini.
Amesema pamoja na hatua hiyo, TRA itaendelea kusimamia kwa karibu ili kudhibiti vitendo vya udanganyifu katika biashara ya mafuta.
“Hakuna upungufu wa mafuta nchini. Kama Serikali ilivyosema, mafuta yapo ya kutosha. Changamoto zilizoripotiwa hazihusiani na uhaba,” amesema Mwenda.
Mwenda pia amewataka wafanyabiashara kushirikiana na TRA ili kuhakikisha huduma ya saa 24 inatekelezwa kikamilifu na kurahisisha usambazaji wa mafuta nchini.



0 Comments