Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam. Serikali imesema mradi wa uwekezaji wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Mzizima Towers unaotekelezwa jijini Dar es Salaam na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umefikia asilimia 91 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo Desemba 31, 2026.
Taarifa hiyo imetolewa Machi 16, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, alipowasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.
Kwa mujibu wa Waziri Sangu, mradi huo wa uwekezaji unahusisha ujenzi wa minara miwili, ikiwemo mnara wa biashara wenye ghorofa 35 na mnara wa makazi wenye ghorofa 32, ukiwa na jumla ya eneo la ujenzi la mita za mraba 95,018.15.
Amesema majengo hayo yamebuniwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya usanifu wa kimataifa ili kukidhi mahitaji ya biashara, makazi na huduma za utalii katika jiji la Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa mradi huo utakapokamilika utakuwa na hoteli ya hadhi ya nyota tano itakayoendeshwa na Radisson Hotel Group, yenye jumla ya vyumba 156 vya kulala pamoja na vyumba 132 vya makazi ya muda mfupi (hotel apartments).
Mhe. Sangu alisema mradi huo unatekelezwa kwa asilimia 100 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kama sehemu ya mkakati wa Mfuko huo kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati yenye tija kwa wanachama na taifa kwa ujumla.
Alibainisha kuwa uwekezaji huo unalenga kuongeza thamani ya mali za Mfuko pamoja na kuimarisha uwezo wake wa kulipa mafao kwa wanachama.
Akizungumza baada ya ziara ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Hawa Mchafu Chakoma, alisema wajumbe wa kamati wanamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua mradi huo uendelee kutekelezwa ili uweze kuleta tija kwa Mfuko na Taifa kwa ujumla.
“Sisi kamati tumefika hapa na kujionea kazi inayofanyika katika mradi huu. Kazi ni nzuri sana na inaonesha kuwa uongozi wa NSSF chini ya Mkurugenzi Mkuu, Bw. Masha Mshomba, umekuwa mfano wa kuigwa katika usimamizi wa miradi,” alisema Mhe. Hawa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, aliwashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa kufanya ziara ya kikazi na kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika mradi huo.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mhe. Kafiti Kafiti waliipongeza NSSF kwa uwekezaji wa mradi huo mkubwa unaotarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Naye Mhe. Kangi Lugola alisema mradi wa Mzizima Towers ni uwekezaji muhimu wenye tija kubwa kwa Mfuko na Taifa kwa ujumla, akimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF kwa usimamizi mzuri wa Mfuko na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mradi wa Mzizima Towers unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kiuchumi ikiwemo kuongeza mapato ya Mfuko na Serikali, kuimarisha sekta ya biashara na utalii jijini Dar es Salaam pamoja na kuongeza ajira, ambapo zaidi ya wafanyakazi 300 wameajiriwa wakati wa ujenzi wa mradi huo, huku ajira zaidi ya 250 zikitarajiwa kupatikana mara baada ya kuanza kwa shughuli za hoteli na biashara ndani ya jengo hilo.

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
0 Comments