Na mwandishi wetu, Arusha.
Serikali imehamasisha mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kundi la vijana katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii ya Tengeru.
Hamasa hiyo imetolewa leo 02 Machi 2026, na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga katika ziara yake ya kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa Afua za VVU na UKIMWI katika vyuo vya kati na Vyuo Vikuu Jijini Arusha.
Mhe. Nderiananga, ameipongeza Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa kazi kubwa ya kusimamia utekelezaji wa Afua za VVU na UKIMWI waliofanya kwenye Taasisi 26 za vyuo vya kati na Vyuo Vikuu nchini, na kuwapongeza vijana wa Vyuo hivyo kwa kupambana nakuchukua tahadhali na kuzungatia elimu ya kinga na maambukiz ya Virusi vya UKIMWI waliyoipata kupitia wataalam mbalimbali.
Pia, Mhe. Nderiananga amesisitiza kundi la vijana haswa wa Kiume kuhamasika katika upimaji ili watambue hali za Afya zao na kuhimiza Ufuasi mzuri wa Dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kwa waathirika wapya, lakini pia amewapongeza Waathirika wote wa VVU kote nchini kwa matumizi sahihi ya ARV.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Mwitikio wa Kitaifa wa UKIMWI kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Bi Audrey Njelekera, amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kupitia takwimu zilizopo inamipango madhubuti ya kupunguza na kutokomeza maambukizi ya VVU na UKIMWI nchini kote.
Ameongeza kuwa, takwimu zinaonyesha kuwa kundi la vijana kuanzia miaka 15 hadi 24 ndio linaloathirika zaidi na maambukizi mapya hivyo TACAIDS imeanzisha Klabu za kijamii kwenye vyuo vya kati na vikuu ili kusaidia kupunguza unyanyapaa, kuongeza idadi ya wanafunzi kupima na kuongeza ushiriki wa wanafunzi katika mapamabano dhidi ya VVU. Vilevile, kuanzisha programu mbalimbali za kuhamasisha na kuelimisha kupitia mijadala, kuandika machapisho, vibonzo, picha mjongeo na kampeni za kwenye mitandao ya kijamii.
Naye, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Dkt. Eliakira Nnko amesema kuwa, Chuo kinaendelea kuweka mipango na mikakati ya utekelezaji wa Afua za UKIMWI mahali pakazi kwa watumishi na wanafunzi wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, lengo kuu ni kuhakikisha Wanafunzi na watumishi wanabaki na Afya njema, Kupunguza vifo na kutokomeza unyanyapaa ili kuimarisha utendaji kazi na kuweka mazingira salama kwa watumishi na wanafunzi.











0 Comments