Ticker

6/recent/ticker-posts

VETA SHINYANGA YAENDELEA KUWA INJINI YA UJUZI NA AJIRA KWA VIJANA



 Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Richard Mbughuni akizungumza na waandishi wa habari Machi 2, 2026 ofisini kwake kuhusu fursa zinazopatikana chuoni hapo ambazo zinaweza kuleta mabadiliko chanya kwa maisha ya vijana katika kupata ajira na kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi kupitia ujuzi watakaoupata.

Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Richard Mbughuni akizungumza na waandishi wa habari.


Na Kadama Malunde, Shinyanga

Chuo cha Ufundi Stadi Shinyanga (VETA) kimeendelea kujidhihirisha kuwa kitovu cha mapinduzi ya kiuchumi kwa vijana wa Mkoa wa Shinyanga kupitia upanuzi wa mafunzo ya ufundi stadi yanayolenga kuwawezesha kiujuzi, kuwaajiriwa na kujiajiri, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chuo hicho kinaamini kuwa dunia ya sasa haihitaji vyeti pekee bali uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo, kwa kuwa ujuzi ni mtaji, ujuzi ni ajira, ujuzi ni kujitegemea na ujuzi ni heshima.

Akizungumza na waandishi wa habari Machi 2, 2026 ofisini kwake kuhusu fursa zinazopatikana chuoni hapo ambazo zinaweza kuleta mabadiliko chanya kwa maisha ya vijana katika kupata ajira na kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi kupitia ujuzi watakaoupata, Mkuu wa Chuo hicho, Abraham Richard Mbughuni, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka msisitizo mkubwa katika elimu ya ufundi stadi kama nguzo muhimu ya ajira na maendeleo ya taifa.
Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Richard Mbughuni.

VETA NI MSINGI WA TANZANIA YA WATENDAJI

Amefafanua kuwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ni wakala wa Serikali ulioanzishwa kwa Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Sura ya 82, ukiwa na jukumu la kutoa, kugharamia na kuratibu mafunzo ya ufundi stadi nchini.

“Kwa lugha rahisi zaidi, VETA ndiyo inazalisha watu wanaojenga Tanzania kwa vitendo. Nyumba tunazoishi, barabara tunazopita, umeme tunaotumia, mashine viwandani, huduma za utalii, teknolojia za kilimo hadi matengenezo ya magari, yote yanategemea mafundi stadi,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Chuo, dira ya VETA ni “Tanzania yenye Mafundi Stadi Mahiri na wa Kutosha,” huku kaulimbiu ikiwa ni “Ufundi Stadi, Fursa Kama Zote, Kwa Watu Wote.”
UDAHILI WAONGEZEKA MARA MBILI

Katika kupanua fursa kwa vijana, VETA Shinyanga imeongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka. Kabla ya upanuzi wa miundombinu kupitia mradi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) mwaka 2010, chuo kilikuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wapatao 400 wa kozi za muda mrefu na chini ya 1,200 wa kozi za muda mfupi kwa mwaka.

Kwa sasa, udahili umeongezeka hadi wanafunzi 545 wa kozi za muda mrefu na zaidi ya 3,000 wa kozi za muda mfupi kwa mwaka.

Ubora wa mafunzo yanayotolewa umevuka mipaka ya Tanzania, ambapo wanafunzi wa kozi za muda mfupi kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati wamekuwa wakijiunga na chuo hicho, na wengi wao kupata ajira ndani na nje ya nchi.

KOZI ZINAZOENDANA NA SOKO LA AJIRA

Mbughuni amesema chuo kimeboresha na kuanzisha kozi zinazoendana na mahitaji ya soko la ajira hususan katika sekta za madini, ujenzi na biashara ndogo ndogo zinazokua kwa kasi Shinyanga.

Kozi hizo ni pamoja na Umeme wa Majumbani na Viwandani, Uashi, Useremala, Ushonaji na Ubunifu wa Mavazi, Uchomeleaji na Uundaji Vyuma, Ufundi Mitambo, Ufundi Mitambo Mizito, Uhazili na TEHAMA, Ukataji na Ung’arishaji wa Madini Vito pamoja na Ufundi Bomba.
Aidha, kutokana na mwelekeo wa soko la ajira, chuo kimeanzisha kozi mpya za Ufundi Magari, Umeme wa Magari pamoja na Utengenezaji na Ukarabati wa Barabara.

MAFUNZO KWA MAKUNDI MAALUM NA MIRADI MIKUBWA

Chuo pia kimekuwa mstari wa mbele kutoa mafunzo kwa makundi maalum ikiwemo vijana wasio na ajira, wanawake na vikundi vya ujasiriamali.

Kupitia Programu ya Wanawake na Samia, washiriki 368 walipata mafunzo ya stadi mbalimbali, huku Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) ukiwahusisha washiriki 20 (wanaume 16 na wanawake 4) waliopatiwa mafunzo kulingana na mahitaji ya mradi huo.
Lengo ni kuwawezesha kiujuzi na kiuchumi ili waweze kujiajiri au kuajiriwa na hivyo kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa.

USHIRIKIANO NA VIWANDA NA URASIMISHAJI UJUZI

Katika kuhakikisha wahitimu wanakuwa tayari kwa soko la ajira, VETA Shinyanga imeimarisha ushirikiano na migodi, makampuni ya ujenzi, karakana binafsi na taasisi za umma kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo (IPT) na mfumo wa Uanagenzi Pacha (DATS).
Pia chuo kinaendesha mpango wa Urasimishaji Ujuzi (Recognition of Prior Learning – RPL) kwa mafundi waliopata ujuzi nje ya mfumo rasmi. Mafundi hao hupimwa na kupewa vyeti vinavyotambulika kitaifa, hatua inayowawezesha kushiriki zabuni za Serikali na kupata ajira rasmi.

UNYUMBUFU NA UBORA WA MAFUNZO

Chuo kinapokea waombaji wote bila ubaguzi, wakiwemo wahitimu wa elimu ya juu wanaotaka kuongeza ujuzi wa vitendo (hands-on skills) ili kujiimarisha zaidi kiushindani katika soko la ajira.

Serikali imeendelea kuboresha karakana, madarasa na vifaa vya kisasa vya kufundishia, huku watumishi wakipewa mafunzo ya kuongeza umahiri ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko.

UJUMBE MZITO KWA VIJANA

Katika ujumbe wake kwa vijana, Mbughuni amesisitiza kuwa dunia ya leo haihitaji vyeti pekee bali uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo.

“Ujuzi ni mtaji, ujuzi ni ajira, ujuzi ni kujitegemea na ujuzi ni heshima. Hivyo ninawahamasisha vijana wote kuja VETA Shinyanga kujifunza stadi mbalimbali ili wajiajiri na kuajiri wengine”, amesema.

VETA – INJINI YA AJIRA NA UCHUMI SHINDANI

Mkuu huyo wa Chuo amesema kupitia uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita, VETA imekuwa injini ya kuzalisha ajira na uchumi shindani.

Ameomba wanahabari kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu fursa zinazotolewa na chuo hicho ili kila kijana ajue kuwa mustakabali wake uko mikononi mwake.

“Tunatambua kuwa Ufundi Stadi, Fursa Kama Zote, Kwa Watu Wote. VETA Shinyanga, Kazi Mkononi,” amesema Mbughuni.

Post a Comment

0 Comments