Na William Bundala-Kahama Shinyanga
Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani wafanyakazi wanawake wa taasisi ya kuzia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga wametoa misaada ya chakula na mahitaji mengine kwa wazee wasiojiweza katika Kata ya Uyogo halmashauri ya Ushetu na kuchangia shilingi laki tano ya ujenzi wa shule ya Sekondari Uyogo.
Wakikabidhi misaada hiyo katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Uyogo Mwamba Masanja ambaye ni naibu Kamanda wa Takukuru mkoa wa Shinyanga amesema kuwa wameamua kutumia maadhimisho ya siku ya wanawake wameamua kuwatembelea wazee ili kuwapa elimu ya kupambana na rushwa na kutoa misaada hiyo Pamoja na kuchangia ujenzi wa Shule.
“Sisi mnaotuona ni wanawake wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga,tumekuja kuazimisha siku ya wanawake duiani Pamoja nanyi ikiwa ni Pamoja na kuwapatia misaada hii midogo kwa ajili yenu wazee wetu” Amesema Bi.Masanja.
Sambamba na hayo Bi Masanja amewataka wazee kuelewa moja ya kazi ya Takukuru ni kufuatilia fedha za serikali ili ziwanufaisha wananchi na kwamba wazee nao wana nafasi ya kutoa taarifa kwa kupiga simu namba 113 pindi wanapoona miradi ya maendeleo inahujumiwa.
“Takukuru pia tunafuatilia fedha za serikali,sisi jukumu letu ni kufuatilia hizo fedha je zimefanya kazi iliyokusudiwa,kwahiyo hata nyinyi wazee wetu mnaweza kutupa taarifa kwa kupiga simu namba 113 kama unaona kuna ubadhilifu wowote katika kata yenu ili sisi tuje kufuatilia matumizi ya hizo fedha” Ameongeza Bi.Masanja.
Kwa upande wake Mratibu wa Takukuru mkoa wa Shinyanga Lucia John amewapongeza wanawake wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa mkoa wa Shinyanga kwa kujitoa kuwasaidia wazee wasiojiweza katika kata ya Uyogo na kwamba taasisi hiyo itaendelea kutoa elimu kwa wazee ili waweze kujua madhara ya Rushwa na kutoa taarifa katika maeneo yao.
“Niwapongeze sana wanawake wa Takukuru mkoa wa Shinyanga kwa kujitoa kuwasaidia wazee hawa,sisi Takukuru tutaendelea kuwafikia wazee na kuwapa elimu ili watambue madhara ya rushwa pia waweze kutoa taarifa kwa taasisi” Amesema Bi. Lucia.
Juma Nzembi na Zainabu Ngenzi ni wazee wa kata hiyo wameishukuru taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) kwa kuwawezesha kupata chakula na mahitaji muhimu na kwamba zamani wazee walisaulika ila kwa sasa wanafikiwa na kupata mahitaji kutoka taasisi mbalimbali za serikali.
“Tunawashukuru sana Takukuru kwa kutukumbuka katika siku hii ya wanawake,Zamani sisi wazee tulikuwa tunasaulika ila kwa sasa tunazishukuru tasisi nyingi za serikali kama Takukuru zinatukumbuka na kutupatia misaada mbalimbali ikiwemo chakula” Wamesema wazee hao mara baada ya kupokea misaada hiyo.
Akitembelea na kukagua mabanda katika maadhimisho hayo Mgeni Rasmi wa maadhimisho hayo ambaye ni mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi.Mboni Mhita ameipongeza taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa juhudi za kusimamia fedha za serikali Pamoja na kutoa elimu ikiwa ni Pamoja na kuanzisha madawati ya kupambana na rushwa katika shule za msingi na sekondari.
“Niwashukuru sana na kuwapongeza Takukuru kwa juhudi zenu,tunaona mchango wenu katika kusimamia fedha za serikali lakini pia hongereni kwa kuanzisha madawati ya kupambana na rushwa katika shule za msingi na sekondari hii itasaidia watoto wetu kufahamu madhara ya rushw wakiwa bado wadogo” Amesema Bi.Mhita.









0 Comments