Ticker

6/recent/ticker-posts

JOWUTA KUTOA TUZO KWA WAFANYAKAZI BORA MEI MOSI

  


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kinatarajia kutoa zawadi kwa wafanyakazi bora katika vyombo hivyo, katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani Mei Mosi ambayo kitaifa itafanyika mkoani Njombe.

Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma Siwayombe ametoa taarifa hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maandalizi ya Mei mosi kitaifa ambayo yatafanyika mkoani Njombe.

Siwayombe amesema mwaka huu, JOWUTA itashiriki kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo baada ya kujiunga na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) mwaka jana.

JOWUTA ilitangazwa kuwa miongoni vya vyama vinavyounda TUCTA katika maadhimisho ya Mei Mosi mwaka jana mkoani Singida, mbele ya Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan baada ya kukidhi vigezo vya shirikisho hilo.

"Kwa mara ya kwanza wafanyakazi bora katika vyombo vya habari tutawapa zawadi katika maadhimisho ya Mei mosi na tayari mchakato umeanza kuwatambua"amesema
Siwayombe amesema, maamuzi ya kuwatambua wafanyakazi bora yamefikiwa na Kamati ya Utendaji wa JOWUTA, ili kuthamini mchango wa wafanyakazi katika vyombo vya habari licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa.

"JOWUTA tuna wanachama zaidi ya 500 nchi nzima ambao wamekuwa wakifanyakazi kubwa sana kuhabarisha umma masuala mbalimbali  ikiwepo ya maendeleo hivyo ni muhimu sana kutambua mchango wao," amesema

Siwayombe ameiomba Serikali na wadau wa wanahabari nchini, kujitokeza kudhamini zawadi za wafanyakazi bora  katika vyombo vya  habari ili kuonesha kuthamini mchango wao kwa umma na kwa kwa taasisi zao.

"Mwaka huu tumepanga kutoa zawadi za kitaifa kwa wafanyakazi bora lakini pia kwa wafanyakazi bora katika baadhi ya mikoa nchini,"amesema

Amewataka waandishi wa habari  nchini kujitokeza kushiriki katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi na kuandika habari, zikiwepo zitakazochochea uboreshaji wa kazi zenye staha nchini ikiwepo kwa wanahabari  wanaokabiliwa na changamoto kadhaa ikiwepo kutokuwa na mikataba ya kazi na kukosa stahili kadhaa .

Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya amesema JOWUTA imeandika maombi ya kuomba ufadhili kwa taasisi kadhaa ambazo zinafanya kazi na vyombo vya habari.

"Kama walimu,madaktari,wafanyakazi sekta binafsi na wengine wanatambuliwa na kupewa tuzo kila mwaka tumeona  wanahabari wanapaswa kutambuliwa tunaomba serikali, mashirika ya umma na makampuni  binafsi kujitokeza kudhamini tuzo za wanahabari bora, amesema

Alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya Mei Mosi  mwaka huu ni "Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050".

Post a Comment

0 Comments