Na Mwandishi Wetu.
Katika juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kikazi na kujionea utekelezaji wa majukumu ya udhibiti wa ubora wa bidhaa nchini, Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Zanzibar inayoshughulika na Utalii, Biashara na Kilimo Leo April, 17 , 2026 imefanya ziara maalum katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na kujionea kwa karibu namna taasisi hiyo inavyolinda afya za wananchi kupitia usimamizi madhubuti wa viwango.
Ziara hiyo imelenga kutoa uelewa mpana kuhusu mifumo ya udhibiti wa ubora wa bidhaa zinazoingia na zinazozalishwa nchini, pamoja na mchango wa TBS katika kuhakikisha usalama wa walaji.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa kamati walipata fursa ya kutembelea maabara za TBS ambazo ni za kisasa na zenye ithibati ya kimataifa, jambo linaloziwezesha kutoa matokeo yanayoaminika kimataifa, kupitia vifaa vya kisasa na wataalamu waliobobea, TBS imekuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha bidhaa hatarishi haziwafikii wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Bi. Fatma Madoba, ameipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika ndani ya TBS uwekezaji ambao umeongeza uwezo wa taasisi hiyo kusimamia ubora wa bidhaa kwa ufanisi zaidi, na hivyo kulinda afya za Watanzania.
“Tunampongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, kwa maono yao ya kuwekeza katika taasisi hii muhimu. TBS ni nguzo ya usalama wa bidhaa nchini, haya mambo mazuri na makubwa tuliyoyaona ndani ya maabara za TBS , tutaenda kuishauri pia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaweze kuwepo kwenye Taasisi yetu ya ZBS " alisema Madoba.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Zanzibar , Dkt. Habiba Hassan Omary , alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha taasisi za viwango ili kukabiliana na changamoto za soko la kisasa, ikiwemo bidhaa zisizo na ubora zinazoingia nchini.
Alieleza kuwa katika dunia ya ushindani wa kibiashara, ubora wa bidhaa si chaguo bali ni hitaji la lazima.
“Ulinzi wa mlaji unaanza na ubora wa bidhaa. Hatuwezi kuzungumzia maendeleo ya viwanda bila kuweka mifumo madhubuti ya viwango,” alisisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa TBS Dkt. Ashura Katunzi ameipongeza na kuishukuru kamati iyo kwa kufika TBS kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali kupitia maabara za TBS kwa ajili ya kulinda afya za watanzania na kusisitiza kuwa Shirika liko madhubuti katika kupambana na kudhibiti bidhaa zisizokidhi Viwango kuingia nchini pamoja na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya Bidhaa hasa Bidhaa za Pombe kwa watumiaji , Naye Mkurugenzi Mkuu wa ZBS , Yusuph Majid Nassor, alieleza kuwa ziara hiyo imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya ZBS na TBS, hususan katika kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kuoanisha viwango.
Alibainisha kuwa Zanzibar pia inanufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa TBS, hasa katika kuhakikisha bidhaa zinazovuka baina ya pande mbili za Muungano zinazingatia ubora unaotakiwa.
Kwa ujumla, ziara hiyo imeonyesha wazi kuwa TBS si tu Taasisi ya Udhibiti wa Viwango, bali ni mhimili muhimu wa kulinda afya, kukuza uchumi wa Viwanda, na kujenga imani ya watumiaji.
Katika kipindi ambacho masoko yanazidi kupanuka na bidhaa kutoka mataifa mbalimbali kuingia nchini, uwepo wa maabara zenye ithibati ya kimataifa unaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kulinda maslahi ya wananchi wake.









0 Comments