Ticker

6/recent/ticker-posts

SEKTA YA VIWANDA YASHIRIKIANA NA VETA, ENABEL KUANDAA WATAALAMU

Ushirikiano kati ya VETA, Enabel na kiwanda cha Kasulu Sugar umeanza kuzaa matunda baada ya vijana 36 waliokuwa wakifanya kazi bila vyeti kutathminiwa na kupatiwa vyeti kupitia mfumo wa urasimishaji wa ujuzi (RPL).

Meneja Rasilimali Watu wa Kasulu Sugar, Samweli George Aoram, amesema hayo wakati Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alipotembelea kiwanda hicho Aprili 9 hadi 10, 2026.

Amesema hatua hiyo imechangiwa na ushirikiano thabiti baina ya taasisi hizo, akibainisha kuwa pia wanafunzi 20 kutoka VETA Kasulu wanaendelea na mafunzo kwa vitendo kiwandani hapo huku wakichangia uzalishaji.

Aoram amesema kampuni iko tayari kuendeleza ushirikiano huo ili kupata wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya kazi.

Naye Meneja wa Mradi wa Wezesha Binti kutoka taasisi ya Enabel, Christine Karungi, amesema lengo ni kuelewa mahitaji ya waajiri ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanatatua changamoto za ajira kwa vijana.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na viwanda ni nguzo muhimu katika kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.

Amesema ziara hiyo imelenga kujionea mahitaji ya ujuzi viwandani na kuimarisha ushirikiano utakaosaidia kuboresha mitaala ya mafunzo ili iendane na mazingira ya kazi.

Amefafanua kuwa kupitia ushirikiano huo, VETA inalenga kuandaa mitaala inayozingatia mahitaji ya waajiri pamoja na kuongeza fursa za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.

“Ushirikiano wa karibu na viwanda utatusaidia kuandaa wahitimu watakaoanza kazi moja kwa moja bila kuhitaji mafunzo ya ziada,” amesema.

Aidha, amesema hatua hiyo inawajengea uwezo wakufunzi kwa kuwapatia uzoefu wa teknolojia za kisasa viwandani, hali inayoongeza ufanisi wao wanaporejea kufundisha.

Post a Comment

0 Comments