Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuzindua ofisi mpya katika mkoa wa Pwani, na kutoa vyeti na leseni 143 kwa wazalishaji wa bidhaa katika kanda ya mashariki inayojumuisha mikoa ya Pwani, Morogoro na Tanga, Hatua inayolenga kuongeza uzingatiaji wa viwango vya ubora katika uzalishaji wa bidhaa nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi hiyo iliyopo katika jengo la Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Mkoani Pwani Katibu Tawala Msaidizi wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji mkoani humo, Bi. Ritta Magere, amesema uwepo wa ofisi hiyo utarahisisha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma kwa wazalishaji, hasa katika mkoa huo wenye zaidi ya viwanda 1,700.
Bi. Magere ameipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia TBS kwa kuanzisha ofisi hiyo, akieleza kuwa ni hatua muhimu itakayoongeza tija kwa wamiliki wa viwanda na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali katika mkoa wa Pwani na maeneo jirani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema shirika hilo linaendelea kusogeza huduma kwa jamii ili kupunguza adha ya wazalishaji kusafiri umbali mrefu kwenda Dar es Salaam kufuata huduma, Amesema ofisi ya Pwani itakuwa mbadala rahisi kwa wadau wa kanda hiyo.
Aidha, Dkt. Katunzi ameongeza kuwa TBS ina mpango wa kuanzisha ofisi ndogo katika mkoa wa Morogoro ili kuendelea kuwafikia wadau karibu zaidi, hatua ambayo itasaidia kuokoa muda na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Baadhi ya wazalishaji wa bidhaa, akiwemo Bi. Angela Sanga, wamepongeza uamuzi huo wakisema kuwa utaongeza motisha ya kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na kimataifa, huku wakitarajia kunufaika zaidi na huduma zilizo karibu nao.





0 Comments