Na Mwandishi Wetu
JINHUA, CHINA — Taasisi za elimu ya juu kutoka Tanzania zikiwemo ADEM, MUCE, TIA, SUZA na UDSM zimeshiriki Kongamano la 3 la Marais wa Vyuo Vikuu kati ya China na Afrika lililofanyika jijini Jinhua kuanzia Aprili 14 hadi 20, 2026.
Kongamano hilo limewakutanisha viongozi wa vyuo vikuu, wasomi na wadau wa elimu kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kubaini fursa mpya za maendeleo ya pamoja katika sekta ya elimu ya juu.
Kaulimbiu ya kongamano hilo ilikuwa “Mshikamano, Mabadiliko na Uendelevu: Kujenga Mwelekeo Mpya wa Ushirikiano wa Elimu ya Juu kati ya China na Afrika,” sambamba na maadhimisho ya miaka 70 ya Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal (ZJNU).
Akizungumza katika kongamano hilo, Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (ADEM), Dkt. Maulid J. Maulid, aliwasilisha mada iliyolenga kuangazia umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuboresha usimamizi wa elimu nchini Tanzania.
Mada yake ilihusu “Kuanzia Mshikamano hadi Uendelevu: Kufikiria Upya Usimamizi wa Elimu kupitia Ushirikiano wa Pande Mbili kati ya Tanzania na China.”
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye, aliwasilisha mada iliyojikita katika utekelezaji wa ushirikiano wa elimu ya kidijitali, akisisitiza haja ya kuhamisha mikataba ya ushirikiano kutoka kwenye maandishi kwenda katika vitendo vinavyoleta matokeo chanya.
Naye Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Profesa Method Samwel, aliwasilisha mada iliyotambulisha nafasi ya chuo hicho katika kukuza ushirikiano wa kitaaluma na China.
Aidha, Rektor wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Amos Palangyo, pamoja na mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), walishiriki katika mjadala wa meza ya duara uliolenga kujadili kwa kina masuala yaliyoibuliwa katika mawasilisho mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal kiliwateua baadhi ya washiriki kutoka Tanzania kuwa watafiti katika mfumo wa kubadilishana wataalamu na vyuo vikuu kati ya China na Afrika.
Walioteuliwa ni pamoja na Profesa William Anangisye, Profesa William Palangyo, Profesa Method Samwel Semiono, Dkt. Maulid J. Maulid na Dkt. Macha.
Kongamano hilo limehudhuriwa na mamia ya washiriki kutoka nchi mbalimbali, likiwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao ya kitaaluma.
Kupitia ushiriki huo, Tanzania inatarajiwa kunufaika na programu za ubadilishanaji wa wanafunzi na wataalamu, fursa za ufadhili wa masomo, pamoja na kujengewa uwezo katika maeneo ya teknolojia za elimu ikiwemo Akili Unde (AI), usanifu wa ufundishaji, uongozi na ufundishaji wa masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).





















0 Comments