Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) amekutana na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje na Maendeleo ya Kijamii na Familia wa Singapore Mhe. Zhulkarnain Abdul Rahim jijini Port Louis, Mauritius, Aprili 12, 2026 kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kupitia biashara, uwekezaji na maendeleo endelevu.
Mazungumzo hayo yamefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tisa wa Bahari ya Hindi uliomalizika Mauritius Aprili 12, 2026 na kuhudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi zinazopakana na bahari ya hindi.
Kufanyika kwa mazungumzo hayo kutasaidia kuongezeka kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore ambapo Mawaziri wote wawili walielezea umuhimu wa kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na kuubadili kuwa uhusiano unaoleta matokeo halisi ya kiuchumi.
Mawaziri hao pia walieleza nafasi ya kimkakati ya nchi zao kama lango la kikanda ambapo Tanzania ikiwa lango la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, na huku Singapore ikiwa lango la Asia, hali inayofungua fursa za kupanua masoko na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.
Balozi Kombo alieleza dhamira ya Tanzania kuvutia uwekezaji zaidi kutoka Singapore katika sekta muhimu zikiwemo bandari, usafirishaji, miundombinu, teknolojia na miradi inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi, akibainisha kuwa utaalamu wa Singapore unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
Aliongelea sifa ya Singapore duniani katika usimamizi wa bandari na mifumo bora ya uchumi kama maeneo yenye uwezo wa kuleta manufaa ya haraka katika ajenda ya ukuaji wa uchumi kwa Tanzania.
Kwa upande wake, Mhe. Zhulkarnain alieleza utayari wa Singapore kuimarisha ushirikiano na Tanzania kupitia kubadilishana maarifa na ushirikiano wa kiufundi katika maeneo kama ubunifu, urahisishaji wa biashara, kilimo, usalama wa chakula na maendeleo endelevu.
Mawaziri hao pia walijadili masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja, yakiwemo usalama wa bahari, biashara ya kimataifa na uchumi wa buluu, wakikubaliana kuendeleza mawasiliano ya karibu kupitia majukwaa ya kikanda na kimataifa huku wakionesha matumaini juu ya mustakabali wa uhusiano wa pande mbili.













0 Comments