MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ((DCEA), imefanikiwa kukamata lita 66,048 za kemikali bashirifu zilizokuwa zikiingizwa na kusafirishwa nchini kinyume cha sheria, katika operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Aprili mwaka huu.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo Mei 13, 2026 jijini Dar es Salaam, Kamishina Jenerali wa Mamlaka hiyo Aretas James Lyimo amesema kemikali zilizokamatwa ni pamoja na lita 16,048 za Cyclohexanone pamoja na lita 50,000 za Extra Neutral Alcohol (ENA), ambazo zinatajwa kuwa na matumizi halali viwandani lakini pia hutumiwa vibaya katika utengenezaji wa dawa za kulevya kwenye maabara bubu.
Amesema operesheni hiyo ilifanyika kwa ushirikiano kati ya mamlaka hiyo, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambapo pia magari mawili yaliyokuwa yakisafirisha kemikali hizo yalikamatwa na watuhumiwa wawili kushikiliwa kwa mahojiano zaidi.
Kwa mujibu wa Kamishina huyo, uchunguzi umebaini kuwa kemikali aina ya Cyclohexanone ziliingizwa nchini na kampuni ya Kinglion Investment Company LTD bila kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kukosa vibali kutoka mamlaka husika.
Aidha ameongeza kuwa kemikali aina ya Extra Neutral Alcohol (ENA) zilikuwa zikisafirishwa kwa kutumia magari ya mafuta aina ya Petrol yaliyokuwa yamebandikwa vibali vya kughushi, hali inayotajwa kuwa ni sehemu ya mtandao wa kihalifu unaolenga kuzichepusha kemikali hizo kwa matumizi haramu.
Kamishina Lymo alieleza kuwa kemikali aina ya Cyclohexanone hutumika kuzalisha dawa za kulevya aina ya Phencyclidine (PCP), na kwamba kiasi kilichokamatwa kingeweza kuzalisha takribani tani 11.4 za dawa hizo haramu.
Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo ilisema sambamba na operesheni hiyo, ilifanya misako katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Morogoro, Dodoma, Njombe, Ruvuma, Kilimanjaro na Mtwara ambapo tani 5.733 za bangi, tani 1.67 za mirungi pamoja na kiasi cha heroin na cocaine vilikamatwa.
Pia ekari 38.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa huku watuhumiwa 84 wakikamatwa kuhusiana na matukio hayo.
Mamlaka hiyo imeonya kuwa itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu wote watakaobainika kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya pamoja na uchepushaji wa kemikali bashirifu, huku ikiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa zitakazosaidia mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.
0 Comments