Ticker

6/recent/ticker-posts

NIT YAENDELEA KUZALISHA WATAALAM WA MIRADI YA KIMKAKATI

NA EMMANUEL MBATILO

Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeendelea kutoa mafunzo kupitia kozi ndefu 49 zinazolenga kuzalisha wataalam mahiri watakaosaidia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 13, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Waziri Mbarawa amesema katika mwaka wa masomo 2025/2026, chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 19,544 wa kozi ndefu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.5 ikilinganishwa na wanafunzi 17,853 waliokuwepo mwaka wa masomo 2024/2025.

Ongezeko hilo linaonesha kuendelea kuimarika kwa mahitaji ya taaluma za usafirishaji, huku NIT ikiendelea kuwa miongoni mwa vyuo vinavyozalisha wataalam wenye ujuzi wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira na miradi ya kimkakati ya taifa.

Kupitia kozi hizo, chuo kinaendelea kuwajengea wanafunzi uwezo katika sekta mbalimbali ikiwemo usafirishaji, uhandisi, urubani pamoja na teknolojia zinazochochea maendeleo ya uchumi wa viwanda nchini.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha rasilimali watu ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalam wa kutosha kusimamia na kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ufanisi na ushindani wa kimataifa.

Post a Comment

0 Comments