Na Adery Masta.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuonesha dhamira yake ya kuhakikisha afya na usalama wa watumiaji wa bidhaa mbalimbali nchini vinabaki kuwa kipaumbele, baada ya kufanya kikao kazi maalum cha tathmini ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya TBS na Halmashauri za Mkoa wa Mbeya.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi za TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuanzia Mei 14 hadi 15, 2026, kimewakutanisha maafisa kutoka halmashauri mbalimbali kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa majukumu ya ukaguzi, kujadili changamoto zinazowakabili pamoja na kuweka mikakati mipya ya kuimarisha usimamizi wa bidhaa za chakula, vipodozi na bidhaa nyingine zinazogusa afya za wananchi.
Kupitia kikao hicho, TBS imeendelea kudhihirisha namna taasisi hiyo ilivyo mstari wa mbele katika kusimamia ubora wa bidhaa zinazoingia sokoni, huku ikishirikiana kwa karibu na serikali za mitaa kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa salama na zenye viwango vinavyokubalika.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho leo Mei 15, 2026, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Bw. Steven Edward Katemba, amelipongeza Shirika la Viwango Tanzania kwa kuandaa kikao kazi hicho muhimu, akieleza kuwa hatua hiyo imekuwa jukwaa la kukumbushana wajibu, kubadilishana uzoefu na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
“TBS niwashukuru sana kwa jitihada zenu katika kulinda afya za Watanzania. Shughuli mnazozifanya za usajili wa maduka ya bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na udhibiti wa bidhaa zisizokidhi viwango kutoka ndani na nje ya nchi ni muhimu sana, hasa kwa Mkoa wa Mbeya ambao ni lango la biashara kutokana na mipaka yake na nchi jirani,” amesema Bw. Katemba.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya TBS na Halmashauri kupitia makubaliano ya MoU umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha ukaguzi wa bidhaa kwenye maeneo ya biashara, masoko, maghala na vituo vya usambazaji, hali inayosaidia kupunguza uwepo wa bidhaa bandia au zisizokidhi viwango sokoni.
Kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Katemba pia amewataka maafisa wa halmashauri kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo maazimio yote yaliyofikiwa katika kikao hicho ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Rodney Alananga, amesema kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji endelevu wa makubaliano yaliyopo kati ya TBS na halmashauri zote nchini, yenye lengo la kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi pamoja na kuongeza nguvu katika ufuatiliaji wa bidhaa zinazohusiana na afya na usalama wa jamii.
Amesema TBS imekuwa ikitoa mafunzo na kuwajengea uwezo maafisa wa halmashauri ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za ukaguzi na utoaji elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango.
“Ushirikiano huu una manufaa makubwa kwa taifa. Tunaposhirikiana vizuri na halmashauri, tunarahisisha ulinzi wa afya za wananchi na kudhibiti bidhaa hatarishi kabla hazijawafikia watumiaji,” amesema Bw. Alananga.
Aidha, amepongeza maafisa wa halmashauri kwa ushirikiano wao mkubwa na kujitokeza kushiriki kikao hicho, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha namna walivyo tayari kushirikiana na TBS katika kutekeleza jukumu la kulinda usalama wa Watanzania.
Naye Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Kidunda Salum, amesema kikao hicho kimekuwa na manufaa makubwa kwa maafisa wa halmashauri kwa kuwa kimewawezesha kufahamiana zaidi, kujadili changamoto zinazofanana na kuweka mbinu za pamoja za kuzitatua.
Mbali na mijadala ya kitaalamu, TBS pia ilitoa zawadi kwa halmashauri zilizofanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yaliyoainishwa kwenye makubaliano ya ushirikiano, hatua iliyolenga kuongeza hamasa na ushindani chanya katika utendaji kazi.
Kwa miaka ya hivi karibuni, TBS imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na mamlaka za serikali za mitaa nchini kupitia MoU waliyosaini na Halmashauri zote nchini inayolenga kuboresha udhibiti wa ubora wa bidhaa sokoni, hasa vyakula, vipodozi na bidhaa nyingine zinazogusa afya za wananchi moja kwa moja.
Hatua hiyo imekuwa msaada mkubwa katika kuhakikisha bidhaa zisizokidhi viwango zinabainika mapema na kuondolewa sokoni, sambamba na kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kufuata viwango vya ubora.
Kupitia jitihada hizo, TBS inaendelea kujijengea taswira ya taasisi muhimu katika kulinda afya za Watanzania, kusaidia ukuaji wa biashara salama na kuhakikisha bidhaa zinazotumiwa na wananchi zinakidhi viwango vinavyotambulika kitaifa na kimataifa.























0 Comments