Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, ameipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kuandaa mpango wa kuwapeleka walimu 40 kwenda kusoma Korea Kusini, akieleza kuwa ni hatua muhimu ya kuimarisha ubora wa elimu nchini.
Akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Elimu Mkoa wa Dodoma uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini hapa, Waziri Shemdoe alisema mpango huo unaendana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
“Mpango huu unaonyesha dhamira ya kweli ya kuboresha elimu kupitia uwekezaji kwa walimu. Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi kama hizi,” alisema Profesa Shemdoe.
Mkutano huo uliandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, kwa lengo la kuhamasisha walimu, wanafunzi na watendaji wa halmashauri kuongeza juhudi katika kuboresha ufaulu wa elimu mkoani humo.
Akizungumza katika mkutano huo, Senyamule alisema mafanikio ya Mkoa wa Dodoma kushika nafasi ya pili kitaifa katika ufaulu yametokana na uwekezaji wa kimkakati wa Serikali pamoja na ushirikiano wa wadau wa elimu.
“Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja za walimu, wanafunzi na Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia,” alisema Senyamule.
Mkutano huo uliungwa mkono na wadau mbalimbali wa maendeleo ya elimu, wakiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii la Watumishi wa Umma (PSSSF), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Benki ya NMB pamoja na taasisi ya Global Education Link.
Akizungumza kwa niaba ya wadhamini, Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, alisema taasisi hiyo ndiyo mratibu mkuu wa safari ya walimu 40 kwenda Korea Kusini, ambapo watapatiwa mafunzo ya kimataifa yatakayosaidia kuboresha mbinu za ufundishaji, matumizi ya teknolojia pamoja na usimamizi wa elimu.
Mollel aliwataka walimu waliochaguliwa kuondoa hofu kuhusu taratibu za safari na maandalizi ya kwenda nje ya nchi, akieleza kuwa kampuni hiyo ina uzoefu wa zaidi ya miaka 19 katika uratibu wa elimu na safari za kimataifa.
“Kupata nafasi ya kwenda nje ya nchi ni jambo moja, lakini utaratibu wa safari ni jambo jingine. Tunawahakikishia walimu wote kuwa waondoe hofu, kwani tutaakikisha taratibu zote za safari, visa na maandalizi muhimu vinakamilika kwa wakati,” alisema Mollel.
Alisema kampuni hiyo itasimamia kwa karibu maandalizi ya pasipoti, visa na maelekezo ya safari kwa walimu wote, huku pia ikitoa mafunzo maalum ya namna ya kujiandaa kisaikolojia kwa wale watakaokuwa wanasafiri kwa mara ya kwanza.
“Tunatambua baadhi ya walimu watakuwa wakisafiri kwa mara ya kwanza kupitia nchi kama Dubai, Qatar au Uturuki kabla ya kufika Korea Kusini. Hivyo tutawapa maandalizi maalum kuhusu taratibu za viwanja vya ndege, maisha ya ugenini na mambo muhimu ya kuzingatia wanaposafiri,” aliongeza.
Aidha, alisema Global Education Link itaambatana na walimu hao kupitia timu maalum ya uratibu ili kuhakikisha safari nzima inakuwa salama, yenye utulivu na yenye mafanikio.
“Lengo letu ni kuhakikisha walimu wanapata uzoefu wa kimataifa utakaoongeza ubora wa elimu na ufaulu wa wanafunzi hapa nchini,” alisema Mollel.
Wakati huo huo, Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuboresha elimu kwa kuwapatia walimu mafunzo ndani na nje ya nchi. Tayari walimu 150 wa masomo ya amali wamepatiwa mafunzo nje ya nchi, wakiwemo baadhi kutoka Mkoa wa Dodoma.
Mkutano huo pia uliambatana na utoaji wa tuzo za umahiri kwa walimu, wanafunzi na shule zilizofanya vizuri katika kuongeza ufaulu, hatua inayolenga kuhamasisha ushindani chanya na kuongeza ari ya kufundisha na kujifunza.
Kwa ujumla, wadau wa elimu wameeleza kuwa juhudi hizo zinaweka msingi imara wa kuendelea kuboresha elimu na kuifanya Dodoma kuwa miongoni mwa mikoa kinara nchini.
Picha mbalimbali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, katika Mkutano wa Wadau wa Elimu Mkoa wa Dodoma uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma jana









0 Comments