Muonekano wa Jengo la Utawala katika Shule mpya ya Awali na Msingi Tinde B iliyopo Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Shule mpya ya Awali na Msingi Tinde B iliyopo Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Wa tatu kulia ni Mbunge wa Jimbo la Itwangi Mhe. Azza Hilal Hamad
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita akimkabidhi vifaa vya michezo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Tinde B, Koksina Frank Nyari,vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Itwangi Mhe. Azza Hilal

Muonekano wa sehemu ya majengo katika shule ya Awali na Msingi Tinde B iliyopo Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga
Muonekano wa sehemu ya madarasa katika Shule mpya ya Awali na Msingi Tinde B iliyopo Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amefungua rasmi Shule mpya ya Awali na Msingi Tinde B iliyopo Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, mradi wa elimu uliojengwa kupitia fedha za Mradi wa BOOST kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 342.9 chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hafla hiyo iliyofanyika Ijumaa Mei 15, 2026 imehudhuriwa na viongozi wa Serikali, vyama vya siasa. wananchi pamoja na wadau wa elimu, ambapo RC Mhita amesema shule hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa watoto.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhita ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya elimu na kuwataka wananchi kuitunza miundombinu ya shule hiyo ili iweze kudumu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hii. Madarasa haya ni mazuri sana na shule hii inaenda kubadilisha maisha ya watoto wetu. Naiomba jamii kuitunza shule hii, kwa sababu majengo haya yanahitaji ulinzi na ushirikiano wa wananchi wote,” amesema Mhita.
Amesema Serikali imeendelea kuonesha dhamira ya kweli ya kuimarisha sekta ya elimu kupitia ujenzi wa shule mpya, madarasa, vyoo pamoja na miundombinu mingine muhimu inayowawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora na salama.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita
RC Mhita pia amewataka wahandisi na wataalamu wa Halmashauri kuhakikisha wanazingatia viwango vya Serikali katika utekelezaji wa miradi ya elimu, afya na huduma nyingine za kijamii ili kulinda thamani ya fedha za umma.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amempongeza Azza Hillal Hamad kwa namna anavyowapigania wananchi wa jimbo hilo na kusimamia maendeleo yanayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Itwangi.
“Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge Azza Hilal kwa namna anavyowapigania wananchi wa Itwangi. Sina mashaka na utendaji wake, anawasikiliza wananchi na kuwaletea maendeleo yanayoonekana,” amesema Mhita.
Kwa upande wake, Azza Hillal Hamad amesema wananchi wa Itwangi wanapaswa kujivunia maendeleo makubwa yanayoendelea kutekelezwa na Serikali ya CCM chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya kipindi kifupi tangu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mbunge huyo amewashukuru wananchi wa Jimbo la Itwangi kwa kukiamini Chama Cha Mapinduzi na kumpa ushindi mkubwa katika uchaguzi uliopita, huku akisema ushindi huo umefungua ukurasa mpya wa maendeleo katika jimbo hilo.
“Nawashukuru sana wananchi wa Itwangi kwa kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi na kunichagua kuwa Mbunge wa Jimbo hili pamoja na kumchagua Dkt. Samia Suluhu Hassan na madiwani wa CCM. Kwa niaba ya CCM napiga magoti mbele yenu kuwashukuru kwa kukiheshimisha chama chetu,” amesema Azza Hilal.
Amesema mara baada ya uchaguzi aliahidi kutorudi jimboni mikono mitupu bali kurejea na majibu ya changamoto za wananchi ndani ya siku 100 za kwanza za uongozi wake, huku akieleza kuwa tayari mafanikio mbalimbali yameanza kuonekana.
“Ninasimama hapa kifua mbele kusema kazi zilizofanywa na Rais Samia ndani ya siku 100 zinaonekana wazi. Leo tunafungua shule mpya ya kisasa hapa Tinde B, jambo ambalo linaonesha namna Serikali ilivyojipanga kuwekeza kwenye elimu ya watoto wetu,” amesema.
Mbunge huyo ametoa historia ya eneo la Tinde akieleza kuwa shule ya zamani ya Tinde aliyosoma yeye mwenyewe kuanzia elimu ya awali hadi darasa la saba ilikuwa ikihudumia wanafunzi wengi mno kutokana na ongezeko la watu, hali iliyosababisha Serikali kuona umuhimu wa kujenga shule mpya na ya kisasa.
“Kijiji hiki cha Nyambui kilizaliwa kutoka Kijiji cha Jomu. Mimi mwenyewe nimesoma katika shule ya zamani ya Tinde kuanzia chekechea hadi darasa la saba mwaka 1988. Wakati huo ilikuwa shule moja tu, lakini kutokana na ongezeko kubwa la watu ikafikia kuwa na zaidi ya wanafunzi 2,000 na baadaye kugawanywa kuwa Tinde A na Tinde B,” ameeleza.
Amesema kutokana na kasi ya ukuaji wa mji wa Tinde, Serikali ya CCM iliona umuhimu wa kujenga shule mpya yenye mazingira bora zaidi kwa ajili ya watoto wa sasa na vizazi vijavyo.
“Leo Tinde B mpya ina madarasa mazuri, ofisi nzuri, vyoo vya kisasa, maji ya Ziwa Victoria, umeme pamoja na eneo kubwa linalojitosheleza. Haya ni maendeleo makubwa tunayopaswa kuyatunza kwa nguvu zote. Shule hii ni mpya, hivyo ni vyema tukapanda miti mingi kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kuongeza mandhari nzuri ya shule,” amesema Azza Hilal Hamad.
Mbunge huyo pia amezungumzia utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo katika Jimbo la Itwangi, ikiwemo usambazaji wa umeme vijijini, mradi wa maji ya Ziwa Victoria.
Amesema Serikali tayari imepeleka umeme katika baadhi ya vitongoji huku maeneo mengine yakiendelea kufikishiwa huduma hiyo kupitia usambazaji wa nguzo na miundombinu mingine.
“Vitongoji vyote vitafikiwa na umeme, wananchi msiwe na hofu. Serikali ipo kazini kuhakikisha kila eneo linapata huduma muhimu,” amesema.
Aidha amesema mradi wa maji ya Ziwa Victoria umeendelea kusaidia wananchi wa Nyambui na Tinde kupata huduma ya maji safi na salama, huku maeneo yaliyosalia yakiendelea kufanyiwa kazi.
Akizungumzia miundombinu ya barabara, Azza amesema Serikali tayari imetoa Shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa dharura wa barabara ya Tinde–Buchama–Usule ambapo mkandarasi ameanza kazi ya ujenzi wa madaraja na ukarabati wa barabara hiyo.
Katika hatua nyingine, Azza Hillal Hamad amekabidhi vifaa vya michezo ikiwemo jezi na mipira kwa timu za wasichana na wavulana wa shule za Tinde A na Tinde B, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuibua na kuhamasisha vipaji vya wanafunzi kupitia michezo mbalimbali.
Katika hafla hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Tinde B, Koksina Frank Nyari, akisoma taarifa ya shule amesema mradi huo umejengwa kupitia mpango wa BOOST unaolenga kuboresha mazingira ya elimu nchini.
Amesema shule hiyo imejengwa kwa gharama ya Shilingi 342.9 milioni zilizotolewa na Serikali, ambapo fedha hizo zilitumika kujenga madarasa mawili ya awali, madarasa sita ya msingi, matundu 18 ya vyoo pamoja na miundombinu mingine muhimu ya kufundishia na kujifunzia.
Kwa mujibu wa Koksina, utekelezaji wa mradi huo ulianza rasmi Novemba 6, 2025 kwa kutumia mfumo wa Force Account na kufikia Machi 13, 2026 kiasi cha Shilingi 338,890,427.8 kilikuwa tayari kimetumika katika utekelezaji wa mradi huo huku kazi za mwisho za ukamilishaji zikiendelea.
Amesema shule hiyo inatarajiwa kuhudumia wanafunzi takribani 360 katika mazingira bora zaidi na kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Koksina amebainisha kuwa kwa sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,284, ambapo wavulana ni 692 na wasichana 592 pamoja na walimu 15, wakiwemo walimu wa kiume wanne na wanawake 11.
Aidha, ameiomba jamii kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda na kuitunza miundombinu ya shule hiyo ili iweze kudumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.











0 Comments