Na Grace Msungu Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Kwagilwa Reuben Nhamanilo, amesema kuwa kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kunategemea kwa kiwango kikubwa uwekezaji wa kimkakati katika usimamizi endelevu wa mazingira pamoja na uwezeshaji wa wataalamu wazawa.
Akizungumza Aprili 30, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa harambee ya ujenzi wa makao makuu ya Chama cha Wataalamu wa Mazingira Tanzania (TEEA), Nhamanilo alisisitiza kuwa ukuaji wa uchumi unaolengwa kufikia dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050 lazima uende sambamba na mifumo madhubuti ya kulinda rasilimali za asili.
Alifafanua kuwa Dira ya Taifa 2050 imejengwa katika nguzo tatu kuu—uchumi imara na shindani, maendeleo ya watu na jamii, pamoja na mazingira endelevu—akibainisha kuwa nguzo ya mazingira ndiyo msingi wa kudumu wa nguzo nyingine zote.
“Tunakabiliwa na ongezeko la watu linalotarajiwa kufikia zaidi ya milioni 118 ifikapo mwaka 2050, sambamba na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi. Bila usimamizi madhubuti wa mazingira, ukuaji huu unaweza kuwa chanzo cha uharibifu mkubwa badala ya maendeleo endelevu,” alisema.
Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa, Tanzania inapoteza wastani wa hekta 370,000 za misitu kila mwaka kutokana na shughuli zisizo endelevu kama ukataji miti holela, kilimo kisicho endelevu na matumizi ya nishati isiyo rafiki kwa mazingira. Aidha, athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuathiri sekta muhimu kama kilimo, maji na nishati.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali inaendelea na maboresho ya kisheria na kitaasisi, ikiwemo marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ili kuimarisha mamlaka ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), pamoja na kuimarisha utekelezaji wa tathmini za athari kwa mazingira (EIA) katika miradi yote ya maendeleo.
Sambamba na hilo, Serikali imeanza kuandaa mfumo wa sera ya “local content” katika sekta ya mazingira, hatua inayolenga kuhakikisha wataalamu wazawa wanapata kipaumbele katika miradi ya kitaifa na ile inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo. Hatua hii inatarajiwa kupunguza upotevu wa rasilimali fedha za kigeni na kuongeza ajira kwa vijana wenye ujuzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEEA, Mhandisi Emmanuel Hanai, alisema chama hicho kinajipanga kuwa kitovu cha kitaifa cha kukuza utaalamu wa mazingira kupitia mafunzo ya kitaalamu, utafiti, ubunifu na programu za incubation kwa wahitimu wa vyuo vikuu.
Alieleza kuwa ujenzi wa makao makuu ya chama hicho utatoa jukwaa la kuratibu wataalamu, kuendeleza viwango vya kitaaluma na kuwezesha ushiriki wa wataalamu wa ndani katika miradi mikubwa ya kimkakati.
Akitoa mtazamo wa kimkakati, Mwanzilishi Mfawadhi wa Umoja Conservation Trust (UCT), Bryan Toshi Bwana, alisema kuwa changamoto kubwa inayoikabili sekta ya mazingira si upungufu wa wataalamu, bali ni ukosefu wa mfumo madhubuti wa kuwaunganisha wataalamu hao na fursa zilizopo.
“Tafiti zinaonesha kuwa takribani dola milioni 300 za Marekani hupotea kila mwaka kupitia miradi inayofadhiliwa na wahisani, kutokana na wataalamu wa ndani kutokupatiwa kipaumbele. Hili ni tatizo la mfumo, si la uwezo,” alisisitiza.
Alipendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kitaifa na kikanda wa usajili na uratibu wa wataalamu wa mazingira, utakaowezesha upatikanaji wa takwimu sahihi za wataalamu, kuongeza uwazi katika zabuni za miradi, na kuhakikisha ushiriki mpana wa wataalamu wazawa.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda barani Afrika, hususan ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa kuanzisha mifumo ya pamoja ya kitaaluma, kubadilishana utaalamu, na kutekeleza miradi ya pamoja ya uhifadhi wa mazingira.
Alieleza kuwa historia ya uhusiano imara kati ya Tanzania na Uganda, uliojengwa na viongozi waasisi kama Mwalimu Julius Nyerere na Rais Yoweri Kaguta Museveni, inatoa msingi imara wa kuendeleza ushirikiano huo katika nyanja za kisasa ikiwemo usimamizi wa mazingira na uchumi wa kijani.
“Ushirikiano wa kikanda si chaguo tena bali ni lazima. Changamoto za mazingira hazina mipaka ya kisiasa; zinahitaji majibu ya pamoja, yenye kuunganisha utaalamu, rasilimali na sera,” alisema.
Kwa ujumla, wadau walikubaliana kuwa ili Tanzania na Afrika kwa ujumla kufikia malengo ya maendeleo endelevu, ni lazima kuwe na uwekezaji wa makusudi katika wataalamu wa mazingira, kuimarisha mifumo ya sera na usimamizi, pamoja na kukuza ushirikiano wa kikanda utakaowezesha matumizi bora ya rasilimali na utaalamu uliopo.








0 Comments