Balozi Mobhare Matinyi akimwonesha Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Géant Electronics, Abdelkrim Mebarkia, vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji nchini Tanzania kwenye banda la Tanzania katika Maonesho ya 57 ya Biashara ya Kimataifa ya Algiers (FIA) yanayoendelea nchini Algeria.
Balozi Mobhare Matinyi akipata maelezo ya kitaalam kuhusu uzalishaji wa nyasi bandia zinazotambuliwa na FIFA kutoka kwa Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa kampuni ya Tapidor ya Algeria, Yahia Ballalou (kulia). Kushoto ni Bounouare Adel, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa wa Tapidor.
Balozi Mobhare Matinyi akizungumza na washiriki wa taasisi za Serikali ya Tanzania, Robert Mtendawema (kushoto) ambaye ni Meneja wa Tehama na Takwimu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Gilbert Lyimo (wa pili kulia) ambaye ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Omary Mafita (kulia), Afisa Hesabu Mkuu wa WRRB.
Wageni mbalimbali wakitembelea banda kuu la nchi washiriki kwenye Maonesho ya 57 ya Biashara ya Kimataifa ya Algiers (FIA) yanayoendelea nchini Algeria.***
Algeria, Algiers
Kampuni za Algeria zinazojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za viwandani na kilimo zinatafuta wabia wa kufanya nazo biashara ya mazao na uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini Tanzania.
Kampuni hizo zilizovutiwa kushirikiana na Tanzania zinashiriki katika Maonesho ya 57 ya Biashara ya Kimataifa ya Algiers (FIA) yaliyofunguliwa na Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria mnamo tarehe 22 Juni, 2026, katika Kituo cha Maonesho cha Shirika la Maonesho na Biashara ya Nje la Algeria (SAFEX).
Maonesho haya ndiyo makubwa zaidi miongoni mwa maonesho ya kimataifa nchini Algeria yakiwa yanazishirikisha jumla ya kampuni 731 zinazojumuisha 549 za Algeria kutoka katika kila sekta na kampuni za kigeni 202 kutoka nchi 36 zikiwemo 16 za Afrika.
Akizungumza katika siku ya pili ya maonesho kwenye banda la Tanzania, Balozi Mobhare Matinyi alizitaja kampuni hizo zinazotafuta wabia nchini kuwa ni GISB inayotaka kuuza vifaa vya umeme na kutengeneza nyaya za umeme kwa kutumia shaba ya Tanzania na GETEX inayotaka kununua katani na pamba na kuwekeza katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi.
“Afisa Mtendaji Mkuu wa GISB, Dkt. Mohamed Khelifa, anakuja tena nchini mwezi Julai baada ya ziara yake ya kwanza mwezi Mei 2026 wakati watendaji wakuu wa kampuni tatu tanzu za GETEX wamepanga kuja nchini mwezi Oktoba 2026 kutembelea Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro (KLICL) ili kuona namna ya kushkushirikiana amesema Balozi Matinyi.
Kampuni zingine ni Tapidor inayotengeneza na kuuza mazulia pamoja na nyasi bandia za viwanja vya soka, Optimaflex ya magodoro, Géant Electronics ya bidhaa za umeme, Bellat ya kusindika nyama na ujenzi wa makaazi pamoja na SARL CPC inayotaka kununua dagaa wa baharini na samaki aina ya jodari ambayo Meneja Mkuu wake, Samir Benhamada, ataitembelea Kampuni ya Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) mwezi Julai 2026.Balozi Matinyi aliongeza zaidi kuwa: “Kampuni zingine za Algeria zinataka kununua bidhaa za kahawa, korosho, ndizi, maharage ya soya, mchele, maziwa ya unga na nyama za ng’ombe, mbuzi na kondoo ambazo huliwa kwa wingi nchini Algeria,” akitolea mfano wa sikukuu ya Idi Al-Adha ambapo Serikali ya Algeria iliingiza kondoo milioni moja kutoka nje ya nchi.
Katika maonesho haya Tanzania inatangaza fahari yake ya utalii wa hifadhi, fukwe za bahari, milima, historia ya kale na utamaduni pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta za madini, viwanda, kilimo, nishati na usafirishaji na vilevile mazao ya chakula na biashara.
Mbali ya Ubalozi, taasisi mbili za Serikali ya Tanzania zinazoshiriki ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inayowakilishwa na Meneja wa Tehama na Takwimu, Robert Mtendawema; na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) inayowakilishwa na Kaimu Mhasibu Mkuu Gilbert Lyimo na Afisa Hesabu Mkuu Omary Mafita.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania,
Algiers, Juni 24, 2026.

0 Comments