Ticker

6/recent/ticker-posts

MWENGE WA UHURU WACHAGIZA UPANUZI WA MTANDAO WA MAJI MKWAJA,WAZIRI AWESO ASISITIZA MAJI YAFIKE WA WANANCHI MOJA KWA MOJA




Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang'onda (wa pili kushoto) akizungumza kwenye mradi wa maji wa Mikocheni/Mkwaja. Kushoto kwake ni Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso na kulia kwake ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mhe Ayubu Sebabili


Na Mwandishi Wetu, PANGANI


WAZIRI wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, ameagizi Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, kuunganisha mtandao wa majisafi na salama kwenye makazi ya watu katika kijiji cha Mkwaja.


Mhe. Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Pangani, ameyasema hayo leo Juni 20, 2026 kijijini hapo, alipokaribishwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa upanuzi mtandao wa maji kutoka ‘mradi mama’ uliopo kijiji cha Mikocheni.

Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Raiyan Mohamed Rashid, akimtishwa ndoo ya maji mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mkwaja wilayani Pangani, Mkoa wa Tanga kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji uliofika kijijini hapo kutokea kijiji jirani cha Mikocheni.



Mwenge wa Uhuru wenye kauli mbiu inayosema, “Tanzania ni yetu sote tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo” ulifika kwenye mradi huo wa kwanza baada ya kuingia katika Halmashauri ya Pangani kutokea Handeni.


Mhe. Aweso amesema, kwa vile Mwenge umechagiza maendeleo wilayani humo kwa vipindi tofauti, ipo haja ya kuendeleza hali hiyo kwa kuingiza maji kwenye makazi ya watu, badala ya kuishia kwenye vituo 12 vya kuchotea maji (DPs) vilivyopo Mkwaja.


Amesema, usambazaji majisafi na salama ni utekelezaji wa ahadi za Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumtua ndo mama kichwani.


Kwa mujibu wa Mhe. Aweso, kati ya vijiji 12,333 vilivyopo nchini, 10,758 vimefikiwa na huduma ya majisafi na salama wakati 1,575 vitafikiwa ifikapo 2030.


Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Pangani, Mhandisi Rajab Hussein, amesema upanuzi wa mradi wa Mikocheni ni matokeo ya upatikanaji maji kwa wastani wa lita 480,000 kwa siku, wakati mahitaji ya Mikocheni pekee ni lita 40,000.


Kwa mujibu wa Mhandisi Hussein, mahitaji yaliyobainika kwa matumizi katika kijiji cha Mkwaja ni lita 65,000 kwa siku na kufanya jumla yake kuwa lita 105, hivyo kuwa na lita 375,000 za ziada.

Ni picha ya uzinduzi wa mradi wa maji.

Amesema kupitia upanuzi wa mradi huo, RUWASA imejenga tenki lenye uwezo wa kuchukua lita 90,000 na kuwekwa kwenye mnara wa urefu wa mita sita, hivyo kuwa na uwezo wa kusambaza maji kijijini Mkwaji kupitia DPs zilizopo.


Naye Mwang’onda amesema agizo la Mhe. Aweso kwa RUWASA kuunganisha mtandao wa maji kwenye makazi ya watu ni kuuheshimisha Mwenge na kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Mwang’onda amesema historia imeandikwa kwa Mhe. Rais Dkt Samia kuboresha huduma za kijamii ikiwemo upatikanaji majisafi na salama sehemu kubwa ya nchi.


Kwa hali, Mwang’onda, amehimiza wananchi kuwekeza zaidi katika amani, umoja na mshikamano, ili kufikia maono ya Mhe. Rais Dkt Samia kuwa na maendeleo endelevu.

Post a Comment

0 Comments