Ticker

6/recent/ticker-posts

TWIGA – BARRICK KINARA KUTOA GAWIO KWA SERIKALI 2026, YATOA KIASI CHA SHILINGI BILIONI 221.9

   

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati), akimkabidhi tuzo Meneja Mkazi wa Barrick nchini Tanzania, Dk. Melkiory Ngido (kulia), kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo kupitia utoaji wa gawio kwa Serikali. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Twiga Minerals Corporation, Bw. Mathias Chanila.
Meneja Mkazi wa Barrick nchini Tanzania, Dk. Melkiory Ngido (kulia), akimkabidhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto), hundi mfano (Dummy Cheque). Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Twiga Minerals Corporation, Mathias Chanila.
***

Ubia kati ya kampuni ya Barrick Mining Corporation na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corporation unaendelea kujenga thamani katika uchumi wa Tanzania, ambapo leo migodi ya Barrick nchini imetoa gawio la Shilingi 221,907,320,687 kwa Serikali na kutunukiwa tuzo ya nafasi ya kwanza kwa kuongoza kwa kutoa gawio kubwa mwaka huu.

Hundi ya gawio hilo (Dummy Cheque) imekabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, katika hafla ya Serikali ya kupokea gawio na michango kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma (Gawio Day 2026) iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita, Barrick-Twiga ilitoa gawio la Shilingi bilioni 93.6. Mwaka wa fedha 2022/23 ilishika nafasi ya kwanza kwa kutoa gawio la Shilingi bilioni 84, huku mwaka uliotangulia ikitoa gawio la Shilingi bilioni 53.5.

Migodi inayoendeshwa chini ya ubia wa Barrick na Twiga Minerals nchini ni North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi, ambao upo katika mchakato wa kufungwa na kwa sasa umegeuzwa kuwa Kongani Maalum ya Kimataifa ya Sekta ya Madini inayojulikana kama Buzwagi Economic Special Zone.

Akizungumzia mafanikio hayo, Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, amesema mbali na kutoa gawio kubwa kwa Serikali, Barrick-Twiga imeendelea kuchangia pato la Taifa kupitia ulipaji wa kodi, ushuru, magawio, mishahara na malipo kwa wazabuni wa ndani tangu kuanzishwa kwa ubia huo mwaka 2019.

Ameongeza kuwa uwekezaji wa Barrick kupitia mkakati wake wa maendeleo endelevu unaendelea kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka migodi yake kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), hususan katika sekta za elimu, afya, maji safi na salama pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Aidha, amesema uwekezaji wa kampuni hiyo unaendelea kukuza biashara za ndani kwa kunufaisha wazabuni na wakandarasi wazawa, sambamba na kuongeza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja nchini.

Mafanikio yanayoendelea kupatikana kupitia ubia wa Barrick na Twiga Minerals ni kielelezo cha uchimbaji madini endelevu unaoweka uwiano kati ya uwajibikaji wa kiuchumi, kimazingira na kijamii.

Kwa upande wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongeza taasisi na makampuni ambayo Serikali ina ubia nayo kwa kuendelea kutoa gawio na kuongeza tija katika biashara na uwekezaji kwa manufaa ya Taifa.

Rais Samia amesema ongezeko la gawio kwa Serikali kutoka Shilingi trilioni 1.28 hadi Shilingi trilioni 1.328 linaonesha kuwa uzalishaji wenye tija umeendelea kuongezeka katika mashirika ya umma, taasisi na makampuni kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa.

"Tunakwenda vizuri na ninajivunia kuwa na viongozi wanaoleta matokeo chanya kwa maslahi ya nchi na watu wake (I am very proud of you)," amesema Dkt. Samia.

Amefafanua kuwa ni muhimu kuendelea kuimarisha uongozi na usimamizi wa taasisi ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya Taifa, huku akisisitiza kuwa Gawio Day ni fursa ya kujipima kuhusu uwekezaji wenye tija unaochochea maendeleo ya kweli.

Pia ametoa maelekezo ya kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa makampuni ambayo Serikali ina ubia nayo ili kuhakikisha pande zote zinanufaika kwa maslahi ya Taifa na ustawi wa Watanzania.

Naye Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Gawio Day ni sehemu muhimu ya kuendeleza mageuzi ya kiuchumi na kimkakati yanayolenga utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Profesa Mkumbo amesema kupitia falsafa ya 4R ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mashirika ya umma, taasisi na makampuni ambayo Serikali ina hisa yameendelea kufanya vizuri katika kuchangia gawio na kuongeza mapato ya Serikali.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo iliyokuwa na kauli mbiu "Uwekezaji wenye matokeo ya nguvu ya ushindani wa Dira 2020–2050," Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema tukio hilo lina umuhimu mkubwa kutokana na mchango wa gawio na hisa katika kukuza uchumi na uwekezaji wa Taifa.

Amesema mashirika ya umma na makampuni yenye ubia na Serikali yana mchango mkubwa katika kuboresha huduma za kijamii na kuongeza mapato ya Mfuko Mkuu wa Serikali.

"Mheshimiwa Rais, kwa maelekezo na maono yako juu ya mageuzi ya kiuchumi na kiutawala pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, yameongeza ufanisi katika biashara na kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na ajira hapa nchini," amesema Mchechu.

Post a Comment

0 Comments