Ticker

6/recent/ticker-posts

ALAMA YA UBORA YA AFRIKA YAZINDULIWA RASMI


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, amesema ubora wa bidhaa ni nguzo muhimu katika kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania kwenye soko la kimataifa na kufanikisha azma ya nchi ya kujenga uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Londo ameyasema hayo leo Julai 31, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa Alama ya Ubora ya Afrika (Africa Quality Mark - AQM), mfumo wa pamoja unaolenga kuwezesha bidhaa zinazozalishwa barani Afrika kutambulika kwa alama moja ya ubora, hatua inayotarajiwa kurahisisha biashara na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima katika mipaka ya nchi wanachama.

Amesema utekelezaji wa mfumo huo utapunguza muda na gharama za ukaguzi wa bidhaa katika mipaka, kuongeza ufanisi wa biashara na kuimarisha utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), hivyo kutoa fursa kubwa zaidi kwa wazalishaji wa Tanzania na bara la Afrika kunufaika na soko la pamoja.

"Ubora wa bidhaa si suala la hiari bali ni msingi wa ushindani wa viwanda vyetu. Kupitia Alama ya Ubora ya Afrika, bidhaa za Tanzania zitapata fursa kubwa zaidi ya kuingia katika masoko ya Afrika na duniani kwa urahisi," amesema Londo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa Taasisi ya Ubora Afrika (ARSO), Reuben Onyangero, amesema Alama ya Ubora ya Afrika ni hatua muhimu katika kujenga mfumo unaotambulika wa ubora kwa bidhaa zinazozalishwa barani humo, jambo litakaloongeza ushindani wake katika masoko ya kimataifa.

Amesema ili mfumo huo uwe na mafanikio, ni muhimu nchi za Afrika kuendelea kuimarisha taasisi na mifumo ya ubora, pamoja na kuhakikisha viwango vinatambulika na kuaminika katika nchi zote za bara hilo.

"Nchi zetu zinapaswa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya ubora ili kuongeza imani ya watumiaji na kurahisisha biashara ya ndani ya Afrika," amesema Onyangero.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, amesema uzinduzi wa Alama ya Ubora ya Afrika ni hatua muhimu kwa Tanzania katika kuongeza ushindani wa bidhaa zake ndani ya soko la Afrika.

Amesema mfumo huo utawezesha bidhaa zinazokidhi viwango kutambulika kwa urahisi katika nchi mbalimbali za Afrika, jambo litakalopanua masoko, kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania na kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda.

Dkt. Katunzi ameongeza kuwa TBS itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na kimataifa kuhakikisha wazalishaji wa Tanzania wanazingatia viwango vinavyohitajika ili kunufaika kikamilifu na fursa zinazotokana na Alama ya Ubora ya Afrika na utekelezaji wa AfCFTA.

Post a Comment

0 Comments