Ticker

6/recent/ticker-posts

DC TUKAI AAGIZA SUNGUSUNGU KUDUMISHA AMANI NZEGA


Na Mwandishi wetu, Nzega

MKUU wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Naitapwaki Tukai ameviagiza vikundi vya ulinzi shirikishi maarufu kama sungusungu kuendeleza na kudumisha hali ya utulivu na amani na kutohamasika na kupotezewa muda na baadhi ya watu wanaohamasisha maandamano yasiyo na tija.

DC Tukai ametoa kauli hiyo ya Serikali juu ya wale wanaohamasisha maandamano wakati akizungumza katika mkutano uliofanyika Kata ya Mwangoye wenye lengo la kuweka maazimio ya kuendelea kulinda amani na kukagua vikundi vya sungusungu.

Zaidi ya sungusungu 4,000 wamekaguliwa na DC Tukai katika kuendelea kusisitiza utendaji kazi bora unaozingatia weledi na namna ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Hata hivyo, DC Tukai amewaagiza sungusungu hao kuwakamata wale wote wanahamasisha uvunjifu wa amani na kuwapeleka mbele ya vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua.

"Tuleteeni wale wote wanaotaka kuharibu amani yetu, kwa sababu haiwezekani tujenge shule mtu aje achome moto, tutekeleze miradi halafu mtu ana mambo yake binafsi aamue tu kuleta vurugu hapa, hatuwezi kukubali," amesema DC Tukai.

Ameeleza kwamba kwa niaba ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Mkuu huyo wa wilaya ya Nzega amekabidhi tisheti 500 kwa ajili ya sare ya sungusungu ambapo ni utekelezaji wa ahadi yake kwa kundi hilo la ulinzi shirikishi huku changamoto zingine zikiendelea kutatuliwa hatua kwa hatua.

"Rais amenituma nije niwaletee ahadi yake, nami nimeifikisha kwenu kwa niaba yake, na anawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuimarisha ulinzi kwenye jamii yenu," amesema DC Tukai.

Mtemi wa sungusungu Tarafa ya Mwakalundi Mathias Ngunda amesema suala la maandamano Tabora halina nafasi kutokana na uwepo wa shughuli nyingi za kufanya ili kuzalisha na kuleta maendeleo kwenye jamii badala ya kuandamana kuvunja amani.

"Hapa hatuna huo muda, tuna kazi nyingi za kufanya kama wananchi, kama haitoshi serikali inaendelea kutuletea mahitaji yetu, sasa hatuwezi kuvuruga amani hapa tushindwe kusonga mbele," amesema Ngunda.

Mbunge wa Bukene John Luhende amesema Bukene hakuna tatizo lolote na hata changamoto zilizopo serikali inaendelea kuzifanyia kazi na yeyote atakayekwenda kuhamasisha vurugu atadhibitiwa mara moja.

"Hapa Bukene sisi hatuna muda wa vurugu kwani serikali yetu tuna imani nayo kubwa sana na ahadi ilizoahidi hapa itatekeleza vizuri tu hatuna sababu za kuandamana,na hatutocheka na yeyote atakayekuja hapa kuharibu amani hii" amesema Luhende.

Hata hivyo, ametoa Sh500,000 kwa kila kata ili kutunisha mfuko wa sungusungu na kwamba hatua hiyo ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na sungusungu katika kuleta maendeleo Bukene.

"Sungusungu hawa ni wa mfano kwa ushiriki wao mkubwa katika miradi ya maendeleo katika jamii yetu na kubwa hasa ni kuunga mkono jitahada hizi ili tufike mbali na kwa haraka,na hii ndio aina ya vijana tunaotaka kwenye jamii na sio maandamano tu," amesema Luhende.

Post a Comment

0 Comments