Ticker

6/recent/ticker-posts

FCC YAWAJENGEA WAJASIRIAMALI UWEZO WA KUTAMBUA BIDHAA BANDIA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) kimeipongeza Tume ya Ushindani (FCC) kwa kuendelea kutoa elimu kuhusu utambuzi wa bidhaa bandia na ulinzi wa biashara kwa wajasiriamali, kikisema mafunzo hayo yameongeza uelewa na kusaidia kulinda biashara halali nchini.

Akizungumza baada ya darasa la elimu leo Julai 10, 2026 katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Ushirikiano wa TWCC, Nelson Clevary, amesema ushirikiano kati ya TWCC na FCC umeendelea kuzaa matunda kwa kuwajengea wajasiriamali uwezo wa kutambua bidhaa bandia pamoja na namna ya kulinda bidhaa na biashara zao dhidi ya vitendo vya udanganyifu.

Alisema mwaka huu ni wa tatu mfululizo kwa TWCC kushirikiana na FCC kuendesha mafunzo hayo, huku matokeo yakionyesha kuwa wajasiriamali wengi wameanza kuelewa athari za bidhaa bandia na umuhimu wa kushirikiana na mamlaka husika zinapotokea changamoto zinazohusiana na bidhaa hizo.

"Leo tumepata darasa zuri ambalo limewasaidia wajasiriamali kutambua bidhaa halisi na bidhaa bandia, lakini pia wamefundishwa namna ya kulinda biashara zao ili zisidhurike kutokana na watu wanaoiga au kutengeneza bidhaa bandia kwa kutumia majina ya biashara zao," amesema Clevary.

Amebainisha kuwa ingawa mafunzo yanayotolewa wakati wa maonesho huwafikia washiriki wachache, bado kuna haja ya kupanua wigo wa elimu hiyo ili kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi nchini.

Clevary amesema TWCC ina wanachama zaidi ya 22,000 nchini, hivyo ushirikiano wa karibu na FCC utawezesha elimu hiyo kuwafikia wengi zaidi na kuongeza uwezo wa wafanyabiashara kulinda bidhaa zao na haki za biashara.

Aidha, amewataka wajasiriamali kuendelea kutumia fursa ya mafunzo hayo kujifunza namna ya kutambua bidhaa bandia na kuripoti vitendo vya ukiukwaji vinavyoweza kuhatarisha biashara zao.

Kwa upande wake Mjasiriamali kutoka mkoani Mwanza, Praxeda Mgyabuso, amesema elimu inayotolewa na Tume ya Ushindani (FCC) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) imewasaidia wafanyabiashara na wananchi kutambua tofauti kati ya bidhaa halisi na bidhaa bandia, pamoja na umuhimu wa kulinda biashara zao kupitia usajili wa alama na nembo za biashara.

Amesema awali alikuwa hana uelewa wa kutosha kuhusu madhara ya bidhaa bandia na namna ya kuzitambua, hali iliyowafanya watumiaji wengi kununua bidhaa zisizo halisi bila kufahamu athari zake kwa afya na uchumi.

Amesema elimu hiyo imewafungua macho wafanyabiashara kutambua kuwa pamoja na kuzingatia ubora wa bidhaa, ni muhimu pia kusajili majina na nembo za biashara ili kuzuia watu wengine kuiga bidhaa zao na kutumia utambulisho wao kinyume cha sheria.

"Kwa kweli tumepata elimu kubwa. Wengi wetu tulikuwa tunanunua bidhaa kwa kuangalia bei ya chini bila kujua kuwa baadhi yake ni bandia na zinaweza kuhatarisha afya zetu. Sasa tumeelewa namna ya kutambua bidhaa halisi na umuhimu wa kulinda biashara zetu kupitia usajili wa nembo na majina ya biashara," amesema.

Nae Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma wa FCC, Roberta Feruzi, amesema kuwa maonesho hayo yameipa tume hiyo fursa ya kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwaelimisha kuhusu haki zao pamoja na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.

Pamoja na hayo amesema mbali na kutoa elimu, FCC pia inatoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi wanaotembelea banda lake, ikiwemo kupokea na kushughulikia malalamiko, usajili wa mikataba na huduma nyingine zinazotolewa na tume hiyo.

Post a Comment

0 Comments