Ticker

6/recent/ticker-posts

TIArb YATOA ELIMU YA USULUHISHI WA MIGOGORO YA KIBIASHARA SABASABA

Taasisi ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara kwa Njia Mbadala Tanzania (TIArb) imewataka wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kupata elimu kuhusu njia mbadala za kutatua migogoro ya kibiashara kwa haraka, gharama nafuu na kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza leo Julai,9 2026 kwenye maonesho hayo, Rais wa TIArb, Adereckson Njunwa, amesema taasisi hiyo imejitolea kuhamasisha matumizi ya usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala kama njia bora ya kupunguza migogoro inayochukua muda mrefu mahakamani na kuathiri shughuli za biashara na uwekezaji.

Amesema moja ya majukumu makuu ya taasisi hiyo ni kusimamia na kukuza utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, kuandaa wataalamu wa usuluhishi pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia mfumo huo katika kushughulikia migogoro yao.

"TIArb pia inashirikiana na serikali pamoja na taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika kuendeleza taaluma ya usuluhishi wa migogoro nchini, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji Tanzania,"amesema.

Aidha, amesema taasisi hiyo imeutumia mwamvuli wa Sabasaba kuutangaza Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Usuluhishi wa Migogoro kwa Njia Mbadala, maarufu kama Dar es Salaam Arbitration Week, ambao utawakutanisha wataalamu wa ndani na nje ya nchi kujadili masuala muhimu yanayohusu biashara na uwekezaji.

Kwa mujibu wake, mkutano huo wa siku tatu utajadili mada mbalimbali zinazohusu uwekezaji, matumizi ya rasilimali asili na maendeleo ya miundombinu, huku ukilenga kuonyesha namna usuluhishi wa migogoro unavyoweza kusaidia kuleta uwiano na maendeleo katika sekta hizo muhimu za uchumi.

Amesema siku ya kwanza ya mkutano itajikita katika masuala ya uwekezaji, siku ya pili itajadili matumizi ya rasilimali asili, huku siku ya tatu ikielekeza mjadala wake katika maendeleo ya miundombinu na nafasi ya usuluhishi katika kuimarisha utekelezaji wa miradi mikubwa.

Post a Comment

0 Comments