Ticker

6/recent/ticker-posts

MATOKEO DUNI YACHOCHEA MAFUNZO YA UMAHIRI KWA WANAFUNZI TANGA



Wataalamu waanza kuwanoa wanafunzi, walimu na maafisa elimu kukabiliana na matokeo duni ya mitihani





Na Oscar Assenga, Tanga

MATOKEO duni ya mitihani ya Taifa katika baadhi ya shule za sekondari za Serikali Jijini Tanga yameibua hatua mpya za kuwanufaisha wanafunzi kupitia mafunzo maalumu yanayolenga kuongeza ufaulu kwa kuwajengea uwezo wa kujifunza kwa ufanisi na kujiandaa vizuri kwa mitihani.

Mafunzo hayo yanatekelezwa na Taasisi ya Tanzania Centre for Education (TCE) kwa kushirikiana na Taasisi ya Botnar foundation na Inovex kupitia mradi wa Tanga Yetu, unaohusisha shule 10 zilizobainika kuwa na changamoto ya matokeo hafifu kwa wanafunzi.

Akizungumza wakati wa kuanza kwa mafunzo hayo katika Shule ya Sekondari Nguvumali, Mkurugenzi Mtendaji wa TCE, Yusuf Ogutu, alisema kuboresha ufaulu ni hatua muhimu ya kuinua ubora wa elimu na kuwawezesha wanafunzi kufikia ndoto zao za kitaaluma na maisha ya baadae.

Alisema wanafunzi wengi hufanya mitihani bila kuelewa kwa kina mfumo wa maswali ya umahiri, uzito wa mada na mbinu sahihi za kujibu, hali inayochangia kushuka kwa matokeo licha ya kufundishwa darasani.

"Ndiyo maana tumeamua kuja na mafunzo haya ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa kuelewa, badala ya kukariri. Tunawafundisha namna ya kuchambua muhtasari wa masomo, kutambua mada zinazotiliwa mkazo katika mitihani na kuelewa matumizi ya vitenzi vinavyotumika katika maswali," alisema.



Aliongeza kuwa wanafunzi pia wanapatiwa mbinu za kupanga muda wa kujisomea, namna ya kujiandaa kabla,wakati na baada ya mtihani, jinsi ya kujibu maswali kwa ufanisi na namna ya kujitathmini baada ya kufanya mtihani.

Ogutu alisema mafanikio ya wanafunzi hayawezi kupatikana kwa juhudi za mwanafunzi pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa walimu, wazazi, viongozi wa elimu na wadau wa maendeleo.

"Tunataka kujenga utamaduni wa ufaulu. Mwanafunzi akielewa namna ya kujifunza na mwalimu akapata mbinu bora za kumwelekeza, matokeo mazuri yatapatikana," alisema.

Mbali na mafunzo hayo, alisema taasisi hiyo imeanza kufanya utafiti katika shule zote 27 za sekondari za Serikali za Jiji la Tanga ili kubaini sababu zinazochangia kushuka kwa ufaulu katika mitihani ya Kidato cha Pili na Kidato cha Nne.

Alisema matokeo ya utafiti huo yatawezesha wadau wa elimu kuweka mikakati ya muda mrefu ya kuboresha ubora wa elimu na kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule za Serikali.



Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu Kata ya Nguvumali, Lilian Shetua, alisema mafunzo hayo yanawasaidia wanafunzi kuendana na mahitaji ya mtaala ulioboreshwa unaowataka kuwa wabunifu, wachambuzi na wenye uwezo wa kutumia maarifa katika kutatua changamoto.

Alisema wanafunzi wengi wamekuwa wakifanya mitihani bila kuelewa muundo wake, lakini kupitia mafunzo hayo wanapata uelewa wa namna ya kujiandaa na kujibu maswali kwa kuzingatia matakwa ya Baraza la Mitihani.

"Ni matarajio yetu kwamba elimu hii itabadilisha mtazamo wa wanafunzi na kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule yetu na nyingine zinazoshiriki mradi huu," alisema.



Naye Inspekta wa Polisi wa Kata ya Nguvumali, Sharifu Kiswamba, alisema pamoja na jitihada za kuboresha elimu, bado utoro wa wanafunzi na tabia ya kuzurura mitaani wakati wa masomo vinaendelea kuwa kikwazo kikubwa.

Aliwataka wazazi kuongeza usimamizi wa watoto wao na kushirikiana na walimu pamoja na viongozi wa kata ili kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria masomo na kutumia muda wao kujifunza.



Kwa upande wake, mwalimu wa Shule ya Sekondari Nguvumali, Venosa Massawe, alisema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka kwani yanawasaidia walimu na wanafunzi kutafsiri kwa usahihi matakwa ya mtaala ulioboreshwa.



Hata hivyo, alisema mazingira magumu ya maisha ya baadhi ya wanafunzi, ikiwamo umaskini, malezi yasiyo ya karibu na changamoto za lishe, bado ni miongoni mwa sababu zinazochangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu.



Alisema ushirikiano wa Serikali, wazazi, walimu na wadau wa maendeleo utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kujenga mazingira bora ya kujifunza na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaofaulu kwa viwango vya juu katika mitihani ya taifa.








Post a Comment

0 Comments